Maxime amalizana na Dodoma Jiji, Anicet anahesabu siku

RASMI Dodoma Jiji imemalizana na makocha wake walioisimamia timu hiyo msimu uliopita, ikiwakabidhi barua za kuhitimisha mikataba yao kwa makubaliano ya pande mbili akiwamo aliyekuwa kocha mkuu, Mecky Maxime.

Dodoma Jiji imefikia uamuzi huo baada ya Maxime kuifundisha kwa msimu mmoja tu ikimaliza katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku kocha huyo akiwa bado na mkataba wa mwaka mmoja.

Taarifa kutoka ndani ya Dodoma jiji ni kwamba, Maxime amekabidhiwa barua hiyo juzi baada ya kuomba kuachana kwa makubaliano maalum na viongozi wa timu hiyo huku ikielezwa kocha huyo anarudi Mtibwa Sugar aliyowahi kuichezea na kuifundisha.

Sio Maxime peke yake anayeondoka, inaelezwa wasaidizi wake Nizar Khalfan na kocha wa makipa Peter Manyika nao watakuwa sehemu ya mabadiliko hayo.

“Tumemalizana nao jana (juzi), tumeshampa barua Maxime kwa amani kama ambavyo aliwasilisha maombi hayo, sasa yuko huru na wakati wowote tutatangaza rasmi kwa kutoa taarifa ya klabu.

“Tunataka kuunda benchi jipya kabisa la ufundi maana hata hawa waliokuwa wasaidizi wake kuna nafasi kubwa tutaachana nao, ili kocha atakayekuja aje na watu anaowataka,” kilisema chanzo hicho.

Uamuzi huo ni kama unawasha taa ya kijani kwa kocha Anicet Kiazayidi, kumalizana rasmi na uongozi wa Dodoma Jiji ambao ndio unataka Mkongomani huyo kuwa kocha wao msimu ujao.

Kiazayidi anatajwa kuja na baadhi ya wasaidizi wake ambapo kocha huyo wa zamani wa Tabora United, tayari ameshaanza hesabu za kuunda benchi lake pamoja na kusimamia usajili.