Mwenda ataja mambo matatu kuvuka lengo ukusanyaji mapato Zanzibar

Unguja. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yussuf Mwenda ametaja mambo matatu makuu yatakayotekelezwa ili kufanikisha lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato Zanzibar.

Mwenda amesema kuwa Mamlaka hiyo itaweka mkazo katika kujenga ushirikiano mzuri na wafanyabiashara kwa kurahisisha mazingira ya kufanya biashara, kuimarisha huduma kwa wateja, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi ili waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

“Tutahakikisha tunashirikiana vizuri na walipakodi kwa kurahisisha biashara zao ili wandelee kufanyabiashara na endapo tutafanya hilo tuna uhakika wa kuzidi ongezeko tulilopangiwa na Serikali,” amesema Mwenda .

Mwenda ameyasema hayo leo Jumamosi  Julai 19, 2025 katika uzinduzi wa mkutano wa mwaka wa kutathmini utendajikazi wa Mamlaka hiyo mwaka wa fedha 2024/25 uliofanyika Zanzibar.

Amefafanua, licha ya Mamlaka hiyo kuhitaji kuimarisha utoaji huduma, lakini pia amesema isiwe sababu ya wafanyabiashara kuitumia fursa hiyo kukwepa kulipa kodi na atakaefanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mwenda amesema kuwa Mamlaka hiyo itawagawanya wafanyabiashara katika makundi mbalimbali; wale wanaolipa kodi ipasavyo watawekewa mazingira rafiki ya kufanya biashara; wale wanaolipa kodi kwa kusitasita au kukwepa watachukuliwa hatua stahiki; na kwa wale wanaotaka kulipa kodi lakini hawajui utaratibu, watapewa elimu ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

Hivyo, ameeleza TRA inafanya jitihada hizo kwa sababu wanahitaji wafanyabiashara walipe kodi kwa hiari na sio kushurutishwa na mtu.

Mbali na hayo, Mwenda amesema kupitia mkutano huo wataangaazia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika ukusanyaji wa mapato mwaka uliopita, kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi na kusikiliza changamoto za wafanyakazi kwa kupanga mipango juu ya kutafuta njia bora ya ukusanyaji mapato kisiwani hapa.

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mcha Hassan Mcha amesema kutokana na kukamilika kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa kuvuka malengo ya makusanyo hayo kwa upande wa Zanzibar kwa kukusanya Sh647 billioni sawa na asilimia 27.

Amesema Mamlaka hiyo ilipangiwa kukusanya Sh600 billioni kwa mwaka huo wa fedha, pia mwaka wa fedha 2025/26 wamepangiwa kukusanya Sh825 billioni sawa na ongezeko la asilimia 26. 

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema Mamlaka hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi kwa kuiwezesha Serikali kutoa huduma za kijamii.

Vilevile, amesema TRA imekuwa ni sehemu ya mpango mkakati wa maendeleo kwani inaifanya Zanzibar kukua kwa uchumi wa kasi katika uso wa duniani kwa sababu ya kurahisisha uingizaji wa mizigo visiwani humo.

Hata hivyo, Dk Mkuya ameitaka Mamlaka hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuwa rafiki zaidi kwa umma kwani walio wengi wanaamini kulipa kodi ni kunyang’anywa fedha zao jambo ambalo sio kweli.

“Naipongeza TRA kwa kutoa elimu ya mlipakoji kwa ufasaha zaidi lakini kitengo cha elimu kinapaswa kuongeza juhudi kuwafikia wananchi kwa kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi ili kujenga imani kwa wananchi hao hasa wanaofanyabiashara katika mitandao ya kijamii,” amesema Mkuya 

“Sasa ni wakati sahihi kutafuta njia nzuri ya kudhibiti mapato yanayopotea kupitia biashara ambazo zinafanywa katika mitandao ya kijamii,” amesema.