Mwenge waikubali miradi yote 51 ya Manyara

Hanang. Mwenge wa uhuru mwaka 2025 umepitisha miradi yote 51, iliyokagua, kuzindua, kutembelea na kuweka jiwe la msingi kwenye mkoa wa Manyara, yenye thamani ya Sh71.3 bilioni.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameyasema hayo leo jumamosi Julai 19 mwaka 2025 kwenye eneo la Sagara akimkabidhi mwenge wa uhuru Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendegu.

Sendiga amesema baada ya kuupokea mwenge wa uhuru kutoka mkoa wa Arusha Julai 12 mwaka 2025 ukiwa Manyara, umekimbizwa umbali wa kilomita 1,197.10 kwenye halmashauri saba za Simanjiro, Kiteto, Babati vijijini, Babati mjini, Mbulu mjini, Mbulu vijijini na Hanang’.

Amesema mwenge wa uhuru umeridhia na kupitisha miradi yote 51 ya thamani ya Sh71.3 bilioni kwa kuweka jiwe la msingi katika miradi 11 ya thamani ya Sh9.7 bilioni, kuzindua miradi 16 ya thamani ya Sh5.5 bilioni na kufungua mradi mmoja wa thamani ya Sh98.4 milioni.

Amesema katika mbio hizo za mwenge wa uhuru pia umekagua na kuona miradi 23 ya thamani ya Sh55.9 bilioni.

Ameeleza kwamba katika fedha hizo Sh71.3 bilioni, serikali kuu imetoa Sh62.2 bilioni na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mapato ya ndani imetoa Sh1.9 bilioni, nguvu za wananchi Sh330.5 milioni na wadau wengine Sh6.9 bilioni.

“Miradi hii imegusa sekta ya afya, elimu, maji, mifugo, kilimo, ujenzi wa miundombinu ya barabara, nishati safi, uwekezaji na miradi ya vijana na nawapongeza wana Manyara kwa kuibua, kuanzisha, kuchangia na kuiendeleza miradi hii,” amesema Sendiga.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga (katikati) akiwa na askari wa kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) baada ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego. Picha na Joseph Lyimo



Amesema wakati wa mikesha ya mwenge katika halmashauri saba, watu 1,532 wakiwemo wanaume 1,161 na wanawake 371 walipima maambukizo ya virusi vya ukimwi na watu 10 wanaume watatu na wanawake saba walikutwa na maambukizi.

“Wote waliokutwa na maambukizi wameelekezwa sehemu sahihi za kupata huduma sambamba na na dawa za kufubaza virusi vya ukimwi vilevile jitihada za kupunguza maambukizi mapya zinaendelea ikiwemo kuendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na VVU kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema.

Amesema kwa upande wa mapambano dhidi ya malaria chini ya kauli mbiu ya ziro malaria inaanza na mimi nachukua hatua kuitokomeza, mkoa umegawa vyandarua 87,445 katika kliniki ya wajawazito na vyandarua 39,761 kwa watoto chini ya miaka mitano katika kipindi cha mwaka 2024/2025.

“Katika mkesha wa mwenge jumla ya watu 631 waliweza kupima malaria na miongoni mwao hakuna aliyekutwa na maambukizi ya ugonjwa huo,” amesema Sendiga.

Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi ameupongeza Mkoa wa Manyara kwa miradi mingi ya maendeleo ambayo yote imepitishwa kwa asilimia 100.

Ussi amesema kutokana na ubora wa miradi ya maendeleo iliyopitiwa na mwenge hakuna hata mmoja uliokataliwa hivyo wanastahili pongezi kwa hatua hiyo.

“Tunawapongeza waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara kwa namna walivyotangaza matukio na pia askari wa kikosi cha kuzuia ghasia FFU waliokuwa wanaulinda mwenge walikuwa wakakamavu na wenye hamasa,” amesema Ussi.

Mkazi wa mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara, Charles Bayo amesema mwenge wa uhuru umekuja na fursa mbalimbali za kiuchumi katika eneo hilo.

“Maofisa usafirishaji wakiwa na bodaboda zao wamepata kipato, mama lishe na baba lishe wamepata fedha, nyumba za kulala wageni zimepata wateja hivyo kuwa na mzunguko wa kiuchumi Hanang’,” amesema Bayo.

Kaulimbiu ya mwenge wa uhuru mwaka 2025 ni jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu, mtaji ni afya yako, zingatia unachokula.