Bodaboda waanzishiwa kampeni ya kuepuka ajali

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, limezindua kampeni ya kitaifa ijulikanayo kama “Chuma kwa Chuma Sio Poa”, yenye lengo la kuhamasisha usalama barabarani na kuhimiza waendesha bodaboda na bajaji kuzingatia sheria ili kupunguza ajali za barabarani nchini.

Ajali za barabarani bado zinabaki kuwa changamoto kubwa, hivyo ushiriki wa wadau wanaotoa elimu kuhusu usalama barabarani ni hatua ya kupongezwa na kuungwa mkono na jamii.

Kupitia kampeni hiyo, zaidi ya wasafirishaji 200 katika kila wilaya ya jiji la Dar es Salaam wamefikiwa na mafunzo ya usalama barabarani, huku dhamira ikiwa ni kupanua mafunzo hayo kufikia mikoa yote nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Julai 19, 2025, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura, Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Joseph Mwakabonga, amesema kuwa uzinduzi wa kampeni hiyo unalenga kuwajengea uelewa wa kina waendesha bodaboda na bajaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

 “Kampeni hii ya kutoa elimu ya usalama barabarani kwa bodaboda ni suala mtambuka ambalo kila Mtanzania anatakiwa kuwa sehemu ya kufanikisha. Tunawapongeza wadau kwa kuona umuhimu wa kuwapa elimu hii ndugu zetu wa bodaboda na bajaji,” amesema  Mwakabonga.


Ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuondoa tabia ya kutofuata sheria miongoni mwa waendesha pikipiki na bajaji, kwa imani kuwa wakizingatia sheria ajali zinazotokana na vyombo hivyo vya usafiri zitapungua au kuisha kabisa.

Mbali na kampeni hiyo pia jeshi hilo wamekabidhiwa vibanda vya kisasa na kampuni ya Oryx Energies Tanzania ambapo Mwakabonga amesema vitasaidia askari wa usalama barabarani kutekeleza majukumu yao vizuri kwa kuwa vimefungwa mfumo wa taa za sola.

“Askari polisi kwa kutumia vibanda hivi wanaweza kutekeleza majukumu yao wakati wowote kutokana na kuwa na taa zinazotumia mfumo wa sola, hivyo hata nyakati za giza kazi zetu zitaendelea,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Said Chega amesema ni muhimu kuendelea kupata elimu ya usalama barabarani.

Amesema kampeni ya Chuma kwa Chuma Sio Poa, itawezesha kupunguza ajali barabarani kwa kuwakumbusha madereva kuzingatia sheria.

“Kila siku tunapokea madereva wapya, wapo wa elimu ya msingi na sekondari ambao wanakuja kuungana nasi. Mafunzo kama haya yanatusaidia kujengewa uelewa na kuchukua tahadhari kwa kuheshimu sheria za usalama barabarani,” amesema Chega.

Amesisitiza kuwa elimu kwa waendesha pikipiki ni muhimu kwa kuwa wao husafirisha abiria kila siku, hivyo wanapokuwa na uelewa wa kutosha hata abiria wao wanakuwa salama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania, Imani Mtafya amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya kwa waendesha pikipiki, bajaji na watoa huduma wengine kuhusu usalama barabarani.

Amesema malengo ya kampeni hiyo ni nzuri kwa kuwa na lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia ushirikiano wao na Jeshi la Polisi kwa kutoa michango ya vitendea kazi kama vile vibanda vya kisasa vya askari vinavyotumia nishati ya jua, kofia ngumu, jaketi za kuonekana usiku, vizimia moto na vilainishi bora vya mitambo, pikipiki na magari.

“Natoa mwito kwa wasafirishaji na watumiaji wa pikipiki kuchukua nafasi hiyo kujifunza na kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika jamii zao. Pia vyombo vya habari vina nafasi muhimu sana katika kueneza ujumbe huu, kwani ajali nyingi zinaweza kuzilika,” amesema Mtafya.