Dodoma. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa vibali 164 kwa taasisi na asasi za kiraia kutoa elimu ya mpigakura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025.
Mbali na hilo, pia INEC imetoa vibali vya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu kwa taasisi na asasi za kiraia 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima ameyasema hayo leo Julai 19, 2025 katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari.
“Taasiasi na asasi za kiraia zilizoruhusiwa na kupewa kibali cha kutoa elimu ya mpigakura zitajulishwa kwa njia ya baruapepe kupitia Mfumo wa Usajili ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine ikiwemo kuweka orodha ya watu watakaotoa elimu hiyo,” amesema Kailima.
Kwa upande wa taasisi na asasi za kirai azilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi, zinatakiwa kuwasilisha kwa njia ya Mfumo wa Usajili majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uaangalizi huo kwa ajili ya kuandaliwa vibali.
Kailima amesema taarifa zingine zote muhimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu ya mpigakura na uangalizi wa uchaguzi, miongozo na taratibu zote zitatolewa mapema iwezekanavyo.
“Tunazipongeza taasisi na asasi za kiraia ambazo zimepata kibali cha kutoa elimu ya mpigakura kwa kuwa waangalizi wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani mwaka 2025,” amesema.
Mmoja wa kiongozi wa asasi za kiraia zinazojishughulisha na utetezi wa haki, Musa Juma amepongeza hatua hiyo lakini amesema kutokana na kuchelewa kwa majibu asasi nyingi zitashindwa kufika katika maeneo mengi.
“Nyingi za asasi zilitarajia kupewa majibu mapema ili ziweze kujiandaa kwa rasilimali za kufika katika maeneo lengwa, sasa kwa kuchelewa huku sidhani kama wataweza kufika katika maeneo yote,” amesema Juma.