MICHUANO ya Yamle Yamle Cup inayoendelea kuchezwa Uwanja wa Mao A na B kisiwani Unguja, ipo mzunguko wa pili ambapo imeshuhudiwa jana Ijumaa Julai 18, 2025, JKU Academy ikichomoza na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Al Qaida ukiwa ni mchezo wa Kundi B.
JKU Academy imepata ushindi huo wa pili mfululizo na kuongoza Kundi B kupitia bao la Said Khamis dakika ya 88 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Mao B, ambapo sasa timu hiyo ipo kileleni na pointi sita.
Kwa upande mwingine, Miembeni City imeitembezea Mambosasa City kichapo cha mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mao A, kupitia mabao ya Hassan Nassor dakika ya 63 na Tariq Wakala dakika ya 74.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Miembeni City ikishika nafasi ya pili Kundi B sawa na Al Qaida zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Miembeni City ikiburuza mkia bila pointi.
Katika mechi za Kundi C zilizochezwa jana, Melinne City imeisulubisha Kinazini kwa kipigo cha mabao 5-2. Jafar Neno wa Melinne City alifunga mabao matatu ‘hat trick’ dakika ya 40, 69 na 90, mengine yakifungwa na Miraji Othman (dk 50) na Raizin (dk 75). Mabao ya Kinazini yamefungwa na Fahad Nassor (dk 22) na Hussein Mgaza (dk 46).
Nayo Mwembe Makumbi Combine imeifunga Luxury City mabao 4-1, wafungaji ni Abdallah Muhib (dk 22), Yakoub Said (dk 49), Michael Godlove (dk 63) na Mudrik Abdi (dk 76). Bao la Luxury lilifungwa kwa penati na Haji Wahaji dakika ya 51.
Kwa matokeo hayo, Mwembe Makumbi ipo kileleni mwa Kundi D ikifikisha pointi sita, inafuatiwa na Melinne City iliyokusanya pointi tatu sawa na Luxury FC zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Kinazini ikiwa haina pointi.
Kabla ya mechi za jana, juzi Alhamisi Julai 17, 2025 zilipigwa mechi za Kundi A na C ambapo Mboriborini iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Monduli Combine.
Nassor Kaboka aliifungia Mborimborini mabao matatu dakika ya dakika ya 5, 47 na 60, kisha Yahya Karoa akamalizia la nne dakika ya 80.
Mchenzo wa Kundi A, Kajengwa na Nyamanzi City zilitoka sare ya bao 1-1. Mfungaji wa Kajengwa ni Khamis Hussein dakika ya 34, Haji Khamis Haji akaisawazishia Nyamanzi City dakika ya 77.
Matokeo hayo yameifanya Nyamanzi City kuongoza Kundi A na pointi nne sawa na Kajengwa, zinatofautishwa na mabao ya kufunga na kufungwa, Mboriborini inafuatiwa na pointi tatu, kisha Monduli Combine haina pointi.
Katika michezo ya kundi C, Melitano City iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kundemba FC ambapo Omar Thani aliitanguliza Melitano City kwa bao la dakika ya 32, kisha Abdulrahman Othman akaisawazishia Kundemba dakika 75, kabla ya Shaban Hassan kuipa ushindi Melitano dakika ya 87.
Upande mwingine, Manyalu FC ilitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sokoni Kwerekwe, bao lililofungwa na Mohamed Mussa dakika ya 47.
Msimamo wa Kundi C unaonesha Manyalu ipo kileleni na pointi sita, Kundemba na Melitano City zinafuatia na pointi tatu kila moja, huku Sokoni Kwerekwe haina kitu.
Leo Jumamosi Julai 19, 2025, michuano hiyo itaendelea kwa kucheza mechi za Kundi E na F kukamilisha mzunguko wa pili.
Ratiba upande wa Kundi E inaonesha Wadachi itavaana na Welezo City huku Real Nine City ikikutana na Kipungani, wakati Kundi F ni Pwani Mchangani vs Mazombi FC na Magari ya Mchanga vs B5 FC.
Wakati mzunguko wa pili ukimalizika leo kwa upande wa Unguja, mzunguko wa kwanza wa timu za kisiwani Pemba unatarajiwa kuanza leo ambapo Chake Chake City itavaana na Mkoroshoni na Pochinki City ambao ni mabingwa watetezi wa mashindano hayo itapambana na Ukutini City.