Hapa kuna ndoa au ananihadaa?

Nina uhusiano na mwanamke kwa miaka mitatu na tulipanga mwishoni mwa mwaka huu nikatoe barua kwao na taratibu nyingine ili mapema mwakani tufunge ndoa. Ila nimepata taarifa ana mume na hajawahi kuniambia, si taarifa tu bali hadi picha wakiwa wanafunga ndoa kanisani nimeonyeshwa, ninashindwa kumuuliza atasema ninasikiliza maneno ya watu na ninampenda nahofia kumkosa iwapo nitamkwaza. Nifanyeje na sitaki kumkosa.

Kwanza pole sana kwa kuzama kwenye penzi linakufanya uuogope ukweli.

Katika maisha ya mahusiano, ukweli na uaminifu ni nguzo kuu zinazojenga msingi wa upendo wa kweli na wa kudumu. Ninapata mashaka kama kweli huyu mwenzako mmekuwa kwenye mahusiano kwa miaka mitatu kiasi cha kuelekea kufunga ndoa ana ndoa nyingine, hapa kuna kitu hakipo sawa.

Kwanza hisia zako ni halali, kupenda kwa dhati ni jambo la thamani, lakini linapaswa pia kuambatana na thamani yako kutambuliwa kwa hiari au ulazimishe kwani mapenzi hayana nafasi ya kuondoa utu na thamani yako. Taarifa ulizopewa ni sababu ya kujiuliza maswali ya msingi kuhusu uhalali wa uhusiano wenu. Si jambo dogo kugundua kuwa mtu uliyejitoa kwake kwa upendo na mipango ya maisha ya pamoja anaweza kuwa amekuambia uongo kwa muda mrefu kiasi hicho.

Jiulize amekuficha vitu vingapi, maswali haya yatasaidia hata kuondoa hofu uliyonayo. Simaanishi kila unaloambiwa ni kweli, tuseme hata picha ulizoonyeshwa pengine zimetengenezwa maana hilo linawezekana, lakini ulilolisikia liwe sababu ya kutafuta ukweli ili uwe huru.

Kusita kumkabili kwa hofu ya kumpoteza ni hisia ya kawaida, hasa unapompenda mtu kwa dhati. Hata hivyo, hofu ya kumpoteza mtu haipaswi kukufanya upuuze ukweli au kujifunga kwenye uhusiano wa udanganyifu. Hatua ya kwanza fuatilia kwa njia zako kuubaini ukweli, hakikisha hatua zako za awali hazimuuzi wala kumdhalilisha yeyote.

Ukibaini au vinginevyo hatua muhimu ni mazungumzo ya wazi na mpenzi wako. Hii siyo tu kwa ajili ya kupata majibu, bali pia kujilinda kihisia. Epuka kumshambulia au kumuhukumu mara moja, muulize kwa utulivu na kwa kutumia lugha ya heshima kuhusu taarifa ulizopata. Onyesha kuwa unahitaji kuelewa ukweli  na kama ulipata uhakika katika hatua zako za uchunguzi si vibaya ukitumia mbinu alijue hilo. Kama atakataa kueleza au kujaribu kukupotosha kwa hoja za kukushawishi kuwa unasikiliza maneno ya watu, hiyo ni ishara kuwa hana nia ya kuwa mkweli kwako.

Kama ataeleza na kukiri kuwa ni kweli, basi ni muhimu kutathmini kama kweli unastahili kubaki katika uhusiano huo hata kama wameachana, kwani alipaswa kukueleza hilo mapema kabla hujalisikia kwa watu, yangekuwa mapenzi ya kawaida sawa, lakini hatua mliyofikia kuna baadhi ya vitu ulipaswa kuvijua. Upendo wa kweli haujengwi kwa misingi ya udanganyifu, na huwezi kujenga ndoa imara na mtu ambaye alianza kwa kukuficha jambo la msingi kama ndoa aliyonayo au aliyowahi kuwa nayo. Kujitenga katika hali kama hiyo siyo udhaifu, bali ni hatua ya kujilinda na kujiheshimu.

Kabla hujafanya maamuzi kutokana na jibu lolote utakalopata kutoka kwa mpenzi wako, kumbuka  kuachana na mtu unayempenda si rahisi kuna maumivu lakini ni ya muda. Usiogope kumpoteza mtu aliyekupoteza kwa uongo wake, ogopa kupoteza nafsi yako kwa kumshikilia mtu asiyekuthamini. Kulingana na majibu yake kweli unaweza kuumia, lakini utakuwa huru.