Chan yaingilia uchaguzi TFF | Mwanaspoti

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliopangwa kufanyika Agosti 18 mwaka huu, huenda ukapigwa kalenda kutokana na uwepo wa michuano ya CHAN 2024.

Tanzania ni nchi mwenyeji wa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Agosti 2, 2025 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda ambapo tamati yake ni Agosti 30, 2025.

Katika michuano hiyo, mechi ya ufunguzi itapigwa Agosti 2 kati ya Tanzania na Burkina Faso kuanzia saa 2 usiku, huku mechi zote za kundi B zikipangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Wakati CHAN ikitarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, mchakato wa wagombea wa uchaguzi wa TFF kutangaziwa uamuzi wa kamati ya maadili uliopangwa kufanyika Julai 14 hadi 16, taarifa zinabainisha hakujafanyika huku jana Jumamosi Julai 19 ikiwa ni siku ya mwisho ya kukata rufaa kwa uamuzi wa masuala ya kimaadili kwenye kamati ya rufani ya TFF.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Kiomoni Kibamba alipotafutwa na Mwanaspoti ameweka wazi kuwa hadi sasa hakuna kinachoendelea, huku wao wakisubiri majibu kutoka kamati ya rufani ya TFF.

“Kamati yetu ya uchaguzi ina utaratibu wake, kama muda huu tunasubiri kamati ya rufani ya TFF itupe majibu kwa waliokata rufaa na kupitishwa kama wapo sahihi kuendelea na ndipo tukae kikao ambacho pia kinatakiwa kupangwa na sekretarieti ya TFF,” alisema na kuongeza:

“Kamati ambayo ndio inapanga mkutano huo kwa sasa ipo bize na mambo ya maandalizi ya CHAN hivyo hatufahamu ni lini tutakaa licha ya kwamba inatakiwa mwisho wa mwezi huu tukutane.”

Ikumbukwe kuwa Julai 4 mwaka huu, kamati hiyo ilitoa majina ya wagombea waliopita katika usaili wa awali kisha kufuatiwa na sekretarieti kuwasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya maadili kuanzia Julai 6 hadi 8.

Baada ya hapo, Julai 9 hadi 13 ilikuwa ni kipindi cha kupokea, kusikiliza na kutolea uamuzi masuala ya maadili. Julai 14 hadi 16 ni kutangaza matokeo ya uamuzi wa kamati ya maadili, kisha Julai 17 hadi 19 ni kipindi cha kukata rufani kwa uamuzi wa masuala ya kimaadili kwenye kamati ya rufani ya TFF.

Waliopenya usaili wa awali ni Wallace Karia anayetetea nafasi ya urais akiwa mgombea pekee baada ya wengine watano kukosa sifa. Upande wa wajumbe wa kamati ya utendaji kulikuwa na wagombea 17, lakini sasa wamebaki 10 ambao ni CPA Hosseah Hopaje Lugano, Cyprian Charles Kuyava, Evance Gerald Mgeusa, Issa Mrisho Bukuku, James Patrick Mhagama, Khalid Abdallah Mohamed, Lameck Nyambaya, Mohamed Omar Aden, Salum Ally Kulunge na Vedastus Kalwizira Lufano.