Ukweli wa limbwata kwenye ndoa

Dar es Salaam. “Nimeoa huu mwaka wa saba, lakini nashindwa kumzoea mke wangu, kiasi kwamba nahisi ni kiboko yangu. Nikiwa kazini ninapata shida naona muda hauendi natamani kurudi nyumbani mapema nikamuone kipenzi changu pia nina wivu naye sana.

Naomba kujua hivi kweli duniani kuna limbwata? Nahisi nimewekewa, haya si mapenzi ni wazimu.’’

Huu ulikuwa ujumbe wa kijana mmoja aliyekuwa akiomba ushauri katika jukwaa moja la mtandao wa kijamii, kuhusu hali anayopitia katika uhusiano wake na kumfanya ahisi amewekewa alichokiita kwa jina la limbwata.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili,  limbwata ni dawa ya kienyeji inayopikwa pamoja na chakula aghalabu nyama, ambayo huaminiwa na baadhi ya watu kuwa mwanaume anapopewa na kuila, ina uwezo wa kumpumbaza na kumfanya ajizamishe katika penzi zito kwa mwanamke aliyempa dawa hiyo.

Kwa wengi hufahamu limbwata kama mchanganyiko wa dawa za kienyeji, uchawi au ushirikina unaolenga kuathiri hisia, akili na tabia za mpenzi.

Wapo wanaoamini kuwa linaweza kumfanya mwanaume kuwa mtulivu, mtiifu mno, na asiyeweza kutoka nje ya ndoa.

Shakira Seif mkazi wa Zanzibar anasema baadhi ya wanawake wamejikuta wakijihusisha katika mambo hayo kutokana na ushawishi wa jamaa, ndugu au marafiki wa karibu baada ya ndoa au uhusiano wao kukosa amani na furaha.

“Unaweza kukuta mtu anapitia kipindi kigumu katika ndoa yake baada ya kuomba ushauri kwa watu wa karibu,  wanaweza kuwashauri kwenda kwa waganga ambako wanapewa dawa ambazo wanaamini wakitumia kwa kuzingatia masharti zinaweza kuleta amani katika uhusiano wao”anaeleza.

Hamadi Hamadi mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam anasema sababu ya hali hiyo ni kukithiri kwa matangazo katika mitandao mbalimbali ya kijamii na utitiri wa  matangazo ya waganga wanaodai wana dawa zinazoweza ‘kumtuliza mpenzi.

“Mtu ana changamoto katika ndoa au uhusiano wake asipopata washauri wazuri,  anaweza kujikuta akiingia katika  mtego wa hao waganga wanaodai kutoa dawa ya kumtuliza mpenzi au kurejesha mpenzi aliyeondoka, ”anasema.

Hata hivyo, swali muhimu;  je, ni kweli limbwata lipo? Na ikiwa lipo, lina athari gani katika ndoa au uhusiano?

Akizungumza na Mwananchi, Amina Abdallah mama wa watoto watatu anasema anaamini libwata lipo na linafanya kazi katika uhusiano au ndoa.

Amina anajitolea mfano yeye binafsi kuwa lilimsaidia kufanya mpenzi wake aweze kumuoa kwa haraka.

“Ilipita miaka mitatu tangu anitolee barua bila ya kuleta mahari, wala kufanyika kwa ndoa lakini baada ya kushauriwa kumpa limbwata haikuzidi miezi mitano akatoa mahari na kunioa,”anasema.

Hata hivyo,  kwa upande wake Nyasatu Mdalingwa anapingana na kile alichosema Amina huku akisisitiza kuwa hakuna limbwata au dawa yoyote inayoweza kumtuliza mwenza zaidi ya kuyafanya yale yanayompa furaha na amani.

“Mimi siamini katika uwepo wa limbwata, ninachokijua kuyafanya yale yanayompendeza mwenza wako na kuacha yale yanayomchukiza. Kuwa mbunifu na msafi  ndio silaha pekee zinazoweza kumtuliza mwenza na siyo dawa za namna hiyo,”anasema.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira, Boniventura Mwalongo anasema hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kisayansi unaothibitisha kuwepo kwa limbwata kama dawa ya kienyeji yenye uwezo wa kumdhibiti mwenza kiakili na kihisia.

Hata hivyo,  anasema kinachotokea ni kuwa matumizi ya dawa hizo zinazoaminika na baadhi ya watu kuwa ni limbwata,  zinamfanya mwanamke ajiamini huku akionyesha utii na heshima kwa mwenza wake ili kumshawishi kula au kunywa kile alichokichanganya na limbwata.

“Hakuna mtu asiyependa kuambiwa maneno mazuri na kutendewa yale yanayompa furaha na amani, mtu yeyote anaweza kujenga thamani katika urafiki au uhusiano na mtu kutokana na jinsi anavyoheshimiwa kwa namna anavyopenda aheshimike”anasema.

“Akitendewa hayo lazima mwanaume atatulia, lakini akili na dhana ndani ya akili ya mwanamke inajengeka kuwa kile alichokitumia kwamba  imekuwa sehemu ya nguvu iliyomfanya mwanaume kutulia,”anaeleza.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Neema Mwamkina anayesema hakuna ushahidi wa kisayansi kuthibitisha uwepo au kutokuwepo kwa limbwata,  lakini kisaikolojia anasema unaweza  kujua uimara na udhaifu wa mwenza wako na kisha  kuutumia vizuri katika kumdhibiti.

Mwamkina anasema kumjua vyema mwenza wako ni moja kati ya silaha bora katika kuimarisha uhusiano na kufanya hata baadhi ya watu kuamini kuwa umempa  limbwata.

“Mfano unamjua mume wako anajibu kwa hasira unapomuuliza jambo,  angalia namna nzuri na bora kumfikishia ujumbe wako ili kuepuka ugomvi,”anasema.

Anaeleza kuwa hilo ndilo lilifanya wazee wa zamani kuja na mbinu ya ‘kujaza maji mdomoni’ ili kuepusha kutoa majibu mabaya kwa mwenza wako.

Anasema mwanaume yeyote hata awe mdogo kiasi gani anapenda kuheshimiwa, kusikilizwa na kuthaminiwa.

“Ukishaweza kuwasiliana vizuri na mwenza wako baadhi ya watu wanaweza kudhani kuwa umempa limbwata, ni muhimu sana kuhakikisha unamjua vyema mwenza wako,”anasema.

Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo anasema kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, ni kosa kubwa mno kutumia ushirikina kwa maslahi yoyote katika maisha ya binadamu.

“Iwe kwa sababu ya maslahi ya ndoa, kazi au maisha ya kawaida iwe mwanaume au mwanamke kufanya mambo hayo ni kosa,”anaeleza na kusisitiza kuwa wanaofanya mambo hayo,  ni wazi kabisa hawaifahamu dini vyema na amewashauri kufuata miongozo ya dini.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro,  anasema kiimani ushirikina wa aina yeyote ni mambo ya kishetani na hayafai.

Anasema kwa mujibu wa miongozo ya dini,  pendo linatoka kwa Mungu, hivyo ili liweze kushamiri wahusika lazima wawe watu wanaomcha Mungu, naye atastawisha upendo kati yao.

“Changamoto zozote zinazotokea zinazosababisha mtu kuhisi kutopendwa au kuthaminiwa,  ni vyema kurudi kwa Mungu na kumuomba, ”anaeleza.

Sendoro ambaye pia ni mtaalamu wa saikolojia na malezi,  anasema kisaikolojia baadhi ya wanawake hujikuta wakifanya mambo hayo kutokana na kushindwa kujiamini na kuhisi kama hawatoshi kwa wenza wao.

“Hiyo inawafanya kutengeneza hofu katika ubongo wao na kuona wanakosa vigezo fulani kwa wenza wao,”anasema.

Anasema hilo ni jambo hatari katika ndoa kwani litafanya mtu kujiona kila anachokifanya anakosea hivyo kutengeneza uoga.

Anashauri baada ya mtu kujiingiza katika mambo hayo ni vyema kujitafakari wapi kwenye changamoto kwenye uhusiano wake na kuja na suluhisho sahihi.

Kwa upande wake,  mtaalamu na mshauri wa masuala ya uhusiano, Eva Mrema anasema iwe ni kweli au si kweli, ukweli unabaki kwamba uhusiano wa kweli unapaswa kujengwa juu ya msingi wa uaminifu, mawasiliano, heshima na mapenzi ya dhati na sio imani kama za limbwata.