Mambo manne ya kuwekeza wanandoa

Mwanza. Kuwekeza pamoja katika ndoa ni njia bora ya kuhakikisha kuwa ustawi wa familia inalindwa.

Wanandoa wanaposhirikiana katika mipango ya kifedha, wanajenga msingi madhubuti wa maisha yao na watoto wao.

Makala haya yanaangazia  maeneo muhimu ambayo wanandoa wanaweza kuwekeza kwa faida ya familia:

Elimu                                                      

Elimu ni urithi wa thamani kwa watoto. Wanandoa wanaweza kuwekeza katika mfuko wa elimu kwa watoto wao ili kuhakikisha wanapata elimu bora.

Hii inaweza kuwa kupitia akaunti za akiba, bima ya elimu, au hata mipango ya kufanya malipo ya mapema shuleni.

Wanandoa wanaweza kuwekeza katika kozi za kitaaluma au mafunzo ili kuboresha ujuzi wao na kuongeza kipato cha familia.

Mwalimu Asia Haruna, mkazi wa jijini Mwanza anasema pamoja na elimu bora kutoa ujuzi na maarifa muhimu kwa watoto ambayo yatawamwezesha kupata ajira nzuri, pia huondoa umasikini wa kifikra na kumwezesha mwanandoa kuchakarika kutafuta kipato hata kama asipoajiriwa.

Kununua au kujenga nyumba ni moja ya uwekezaji muhimu kwa familia. Nyumba siyo tu mahali pa kuishi bali pia ni mali yenye thamani inayoongezeka kwa muda.

Wanandoa wanaweza pia kuwekeza katika ukarabati wa nyumba au kuboresha mazingira yake kwa kuongeza thamani na faraja kwa familia.

Afya njema ni msingi wa maisha yenye furaha. Wanandoa wanapaswa kuwekeza katika bima ya afya ili kufidia gharama za matibabu na kuhakikisha huduma bora za kiafya kwa familia nzima.

Pia, wanaweza kuwekeza katika mtindo wa maisha mzuri kama vile  ufanyaji wa mazoezi na kupata ushauri wa mara kwa mara kuhusu afya yao.

Kuanzisha au kuwekeza katika biashara kama wanandoa ni njia ya kuongeza mapato ya familia. Wanandoa wanaweza kushirikiana katika biashara ndogo ndogo kama vile kilimo, biashara ya rejareja, au huduma za kitaaluma. Hii inawapa nafasi ya kujifunza pamoja na kukuza uhusiano wao wakati wanapojenga urithi wa kifamilia.

Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Zacharia Jackson anasema ni muhimu kwa wanandoa kuwa na vyanzo zaidi ya kimoja vya kipato, badala ya kutegemea mshahara pekee.

Anasema kuwa na vipato mbadala kupitia uwekezaji na biashara ni hatua muhimu katika kujenga uthabiti wa kifedha wa familia.

Anaeleza kuwa kihistoria, biashara nyingi zinazoendeshwa na wanandoa au wanafamilia huwa na mafanikio makubwa, na kwa mujibu wa takwimu, nchini Marekani biashara hizo zinachangia asilimia 54 ya pato la taifa (GDP). Aidha, zaidi ya asilimia 70 ya biashara zote duniani zinaendeshwa na wanafamilia.

Kulingana na utafiti wa Family Enterprise USA, biashara za familia zinachangia takriban asilimia 54 ya GDP ya sekta binafsi ya Marekani, sawa na karibu dola 7.7 trilioni, na pia zinawapa ajira asilimia 59 ya wafanyakazi sekta binafsi, yaani takriban watu milioni 83.3.

Dk Jackson anasema mafanikio ya biashara za kifamilia yanatokana na uhusiano wa karibu uliojengwa kwa kuaminiana, maono ya pamoja na hamasa ya kukuza familia.

Anasema ushirikiano huo pia huwapa nafasi ya kupanua maarifa kwa wanandoa wenyewe na hata watoto wao, hivyo kuendeleza mafanikio kutoka kizazi hadi kizazi.

Akiba ni muhimu kwani itawasaidia wakati wa dharura. Wanandoa wanaweza kufungua akaunti ya pamoja ya akiba au kuwekeza katika hisa au miradi ya pamoja. Pia, mipango ya kustaafu ni muhimu kuhakikisha maisha mazuri baadaye.

Akizungumzia faida ya kuweka akiba, Meneja wa Taasisi ya Uwekezaji ya UTT AMIS tawi la Mwanza, Ligwa Temela anasema faida ya kwanza ni usalama wa kifedha, ambapo mtu anayekuwa na akiba huwa na uhakika wa kuwa na kiasi cha fedha kinachoweza kumsaidia wakati wa dharura kama vile maradhi, ajali au matatizo ya kifamilia yanayohitaji fedha za haraka.

“Akiba ni muhimu kwa maandalizi ya maisha ya kustaafu, kwani baada ya kustaafu kipato hupungua na mtu huhitaji kuwa na akiba ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya baadaye,”anasema Temela.

Anasema watu wenye akiba ya kutosha huwa na uwezo wa kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kiuchumi kama vile kununua hisa, kuanzisha biashara au kununua mali zisizohamishika kama ardhi na nyumba.

Hali hiyo huongeza kipato na kuwasaidia wanandoa kutimiza malengo yao ya kifedha kama kununua nyumba, gari au kulipia ada ya shule kwa ajili ya watoto wao.

Temela anaeleza, kuweka akiba huwasaidia watu kuepuka madeni na mikopo isiyo ya lazima, jambo linalopunguza utegemezi wa mikopo yenye riba kubwa ambayo inaweza kuathiri hali ya kifedha kwa muda mrefu.

Aidha, anaeleza kuwa akiba huongeza amani ya akili kwa mtu, pia hujenga tabia ya kujitegemea kifedha na kuwapa watu uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii, kutoa michango kwa wahitaji au kusaidia marafiki na ndugu wanaokumbwa na changamoto za kifedha.

Temela amesema watu wanaoweka akiba mara nyingi huwa na nidhamu nzuri ya kifedha, hujifunza kupanga bajeti, kuepuka matumizi yasiyo ya lazima na kujenga utamaduni wa kujiandaa kwa maisha bora ya baadaye.

Baada ya kazi, kuna haja ya kupumzika. Hapa wanandoa wanaweza kuwekeza pesa ili waburudike wakati wa likizo.

Wanandoa wanaweza kuweka bajeti ya likizo, safari za kitalii, au shughuli za burudani zinazohusisha familia nzima. Hii husaidia kujenga kumbukumbu na kuimarisha uhusiano wa kifamilia.

Wapenzi wanafaa kukumbuka kuwa baada ya kuingia kwenye ndoa, wao ni kitu kimoja na hakuna haja kila mmoja ajishughulishe na masuala yake binafsi.