Dar es Salaam.Tuko baa tunajipoza, mwenzetu mmoja anaweka glasi mdomoni, anagida fundo mbili tattu, anashusha glasi mezani, anakaa kimya sekunde mbili tatu macho kwenye runinga inayoning’inia juu ikionyesha mechi ya ndondi ambayo wala hatuifuatilii.
Kisha baada ya muda anatugeukia na kutuuliza; “Hivi, zawadi gani ya thamani zaidi uliyowahi kumpa mjukuu wako?”
Wote tunamgeukia kumtazama tukimshangaa, tunaelewa swali lake lakini hatuelewi kwanini ameuliza, limetokea wapi? Kwani kati yetu hakuna hata mmoja ambaye ana mjukuu au ambaye hata amefikia umri wa kuwa na mjukuu.
“Kwanini?” Mwenzetu mmoja anamuuliza.
“Tuambie kwanini umeuliza? Hakuna mwenye mjukuu hapa, kwanini unauliza hivyo?”
“Sawa. Ngoja nibadilishe swali.” Anatuambia kisha anauliza swali lake kwa namna nyingine. “Zawadi gani ya thamani zaidi unayoweza kumpa mjukuu wako?”
“Hatuna mjukuu” mwingine anamwambia.
“Najua, najua. Lakini nauliza huko mbeleni, siku ukipata mjukuu.”
Tunamtazama hatumuelewi. Lakini tunagundua ili kujua anapoelekea na hili swali lake ni lazima tumpe anachokitaka… majibu.
“Baiskeli”, “Gemu”, “ada ya shule” kila mtu anamjibu.
Anatutazama, anatabasamu, kisha ananyanyua glasi yake na kugida tena kisha anarudisha mezani.
“Zawadi pekee ya thamani zaidi unayoweza kumpa mjukuu wako ni kuhakikisha hauwi tegemezi kwa mwanao ukizeeka,” anasema na kuendelea:
“Wanaume wa Kitanzania na jamii nyingine katika mataifa yanayoendelea tunateswa sana na mipango ya ovyo ya mababu zetu. Babu alikuwa analewa tu, babu alikuwa anatapanya kila alichokuwa nacho, mwishowe fainali uzeeni inafika, babu hana hata thumni. Hawezi kujihudumia kwa chochote kiuchumi. Matokeo yake anakuwa ni mzigo wa mwanawe.”
“Na mwanawe kwa sababu kipato chake ni kidogo anajikuta analazimika kukigawa kwa ajili ya watoto wake na wewe babu yao. Kwahiyo, kama mwanawo atakuwa na pesa ya kumpeleka mtoto shule nzuri, lakini na wewe unamtegemea, itabidi aigawe hiyo pesa kwako na kwa mjukuu wako, kwahiyo mjukuu wako hataweza kwenda shule nzuri na wewe ndiyo utakuwa sababu.”
Anamaliza kuongea, anachukua chupa anaongeza bia kwenye glasi, ananyanyua glasi anapiga fundo kadhaa.
Wakati anakunywa, namtazama, nawaza, tulikuwa tunaongea mambo ya mpira hapa kabla hatujanyamaza kidogo na yeye kuanza kuongelea mambo ya wajukuu. Lakini alichokiongea kinaningia akilia na kunifanya nijiulize mara mbili mbili, hizi hekima za ghafla zinatoka wapi?
Je, ni mazingira? Kwamba baa kunakuwa na mazingira yanayochochea hekima? Je, ni anachokunywa? Kwamba labda bia zinachochea hekima? Au ni watu wanaokuzunguka?
Kwamba labda sisi rafiki yake tuna hekima sana kwahiyo tumemuambukiza hekima. Jibu sipati lakini ninachoweza kusema ni kweli, zawadi ya thamani zaidi unayoweza kumpa mjukuu wako, ni kutokuwa tegemezi kiuchumi utakapozeeka.
Najua ni ngumu kukata mnyororo wa kuwa tegemezi kiuchumi kwa watoto wako. Wahenga wanasema, siku bora ya kupanda miti ni miaka kumi iliyopita, siku bora nyingine ni sasa.
Kwahiyo kama baba zetu na babu zetu walishindwa, pengine sisi tunaweza kuanza kujipambania kwa kutengeneza mipango ili kuhakikisha watoto wetu wanakuja kutuelea tu, sio kutuhudumia kiuchumi. Tuombe Mungu atusaidie.