Zungumza na mtoto kuhusu fedha

Kuzungumza na watoto kuhusu pesa ni hatua muhimu sana katika kuwasaidia kujenga uelewa wa matumizi bora ya fedha, kuhimiza tabia ya kuweka akiba, na kukuza uhuru wa kifedha kadri wanavyokua. Mazungumzo haya yanapaswa kufanyika mapema, kwa lugha rahisi, na kwa kuzingatia umri na kiwango cha uelewa wa mtoto. Hapa chini ni mwongozo unaoelezea hatua mbalimbali kulingana na makundi ya umri wa watoto.

Anza mapema na kwa mambo rahisi na mepesi yahusuyo pesa. Katika umri wa miaka 3–7, unatakiwa kuwafundisha watoto dhana rahisi kama kuweka akiba, kutumia pesa, na kutoa msaada.

Kama mzazi, washirikishe katika maamuzi madogo ya ununuzi, mfano, kuchagua kati ya pipi mbili au juisi moja na waonyeshe madhara ya kila uamuzi katika kipato. Katika kuwakuza zaidi kwenye eneo la fedha unatakiwa kuwapa vitabu vya hadithi vinavyohusu fedha kwa watoto..

Hii ni muhimu kwa kuwa utafiti umeonesha kuwa tabia za kifedha huanza kuundwa kufikia umri wa miaka saba.

Katika umri wa miaka 8–12; wafundishe kupitia maisha ya kila siku kwa vitendo. Unatakiwa kuwapa nafasi ya kupata pesa kwa kufanya kazi ndogondogo nyumbani. Baada ya kupata pesa hizo wafundishe kugawa pesa katika makundi matatu ambayo ni kuweka akiba, kutumia, na kusaidia wengine kwa mpangilio huo.

Kama mzazi unatakiwa kuwaeleza tofauti iliyopo kati ya mahitaji na matamanio mnapoenda dukani pamoja. katika umri huu, watoto wanaanza kuelewa matokeo ya maamuzi yao. Kuwafundisha vipaumbele husaidia kujiandaa na uamuzi wa kifedha.

Katika umri wa miaka 13-17; wahusishe katika maamuzi halisi. Watoto wa umri huu waingie katika kupanga bajeti ya familia, mfano matumizi ya nyumbani na shuleni.

Mzazi wasaidie kufungua akaunti ya benki au akaunti ya simu ya kuweka akiba na kuwaeleza matumizi ya kadi ya benki, fedha ya kidigitali, na manunuzi ya mtandaoni. Wape fursa ya kutumia kiasi fulani cha pesa kila mwezi kwa mazoezi ya kupanga bajeti binafsi.

Unaweza kutumia michezo na zana za kuelimisha kuwasaidia watoto; kama mzazi unatakiwa kucheza michezo ya kifedha ili kuwafundisha kuhusu pesa kwa njia ya kucheza. Mara nyingi programu hutumika au fomu rahisi za kufuatilia matumizi na akiba. Wahimize kuanzisha biashara ndogo ndogo, mfano kuuza juisi au bidhaa walizotengeneza wenyewe.

Onyesha kwa mfano tabia njema za kifedha;Watoto hujifunza zaidi kwa kuona kuliko kwa kuambiwa. Ikiwa mzazi anapanga bajeti, anaweka akiba, anapima bei kabla ya kununua, au anatoa sadaka kwa wengine, mtoto atajifunza kufanya hivyo pia. Kinyume chake, mtoto huweza kurithi hofu, matumizi mabaya, au msongo wa kifedha kama mzazi hajajipanga vizuri.

Kuzungumza na watoto kuhusu pesa si tukio la mara moja bali ni mazungumzo yanayoendelea. Kwa kutumia lugha rahisi, mifano halisi, na mazungumzo ya wazi, mzazi au mlezi anaweza kuwa msingi wa mafanikio ya kifedha ya mtoto wake kwa maisha yake yote.