Dar es Salaam. Kuimarika kwa huduma jumuishi kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu kumetajwa kuwa sababu ya ongezeko la wanafunzi hao wanaofika elimu ya juu nchini.
Hilo limeenda sambamba na uwekezaji uliofanywa katika maeneo mbalimbali, hali inayochochea kuondoa ugumu wa ujifunzaji na vikwazo vilivyokuwapo.
Takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zinaonesha kuwa idadi ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali wanaofika vyuoni imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 kutoka 1,539 mwaka 2023/2024 hadi kufikia 3,069 mwaka 2024/2025, na kati yao wasioona ndiyo waliongezeka zaidi.
Katika kipindi husika, idadi ya wasioona waliofika elimu ya juu walikuwa 1,559 mwaka 2024/2025 kutoka 740 mwaka uliotangulia, huku walio na usikivu hafifu wakiwa 364 kutoka 189 mtawalia.
Walio na ulemavu wa viungo walikuwa 384 mwaka 2024/2025 ikiwa ni ongezeko kutoka wanafunzi 213 waliokuwapo mwaka uliotangulia, huku walio na matatizo mengine wakifika 647 kutoka 343.
Waliokuwa na ulemavu zaidi ya mmoja walikuwa 61, huku wenye matatizo ya afya ya akili wakiwa 11 katika mwaka 2024/2025.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago, amesema kundi la wasioona linaonekana kuwa na wanafunzi wengi vyuoni kwa sababu walianza kupata elimu tangu enzi za ukoloni, uhuru na hadi sasa wakati ambao Serikali inapambana kuongeza udahili wa watu wenye ulemavu vyuoni.
Amesema hilo limekwenda sambamba na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika ununuzi wa vifaa, ikiwemo vitabu na mashine za kuchapisha nukta nundu kwa ajili yao.
“Vitabu vimeongezeka sana. Zamani baadhi ya masomo yalikuwa hayana vitabu, mtu asiyeona alisubiri asomewe na mwingine ili ajifunze, lakini sasa haipo. Walimu wapo wanaotosheleza kuliko tulipotoka,” amesema.
Amesema pia vyuo vina vituo maalumu vya watu wenye uhitaji, jambo linalorahisisha utoaji wa huduma kwani huwekwa wataalamu na vifaa vyote saidizi vinavyohitajika.
Hata hivyo, ametaka kuangaliwa namna ya kuongeza wataalamu zaidi ili kuwezesha makundi mengine kufikia elimu ya vyuo vikuu kwa wingi zaidi kama ilivyo kwa wasioona.
Hilo litawezekana kwa kutengenezwa kwa mtaala nyumbufu utakaofundishwa kulingana na mahitaji ya mtoto, kwa kile alichokisema kuwa baadhi ya ulemavu hauhitaji mtu kukaa darasani kama wanafunzi wengine.
“Tukifanya hivi tunaweza kuona hata idadi ya wanafunzi wenye matatizo ya afya ya akili wanaongezeka vyuoni, kwani sasa wengi wanaishia shule za msingi na sisi hatutaki wabaki huko pekee,” amesema.
Pia ametaka kutengenezwa kwa miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa viungo ili wapate huduma kwa urahisi, ikiwemo kuwawezesha kupata viti mwendo vitakavyowawezesha kutoka majumbani kwao hadi shuleni.
“Tukifanya hivi watu wenye ulemavu wa viungo watakuwa wengi kwa sababu viti hivi katika baadhi ya maeneo havipatikani kwa wingi na watu hawana uwezo wa kumudu,” amesema.
Katika uwezeshaji wa walimu, ametaka kuangaliwa vyema kwani baadhi ya watu wenye ulemavu bado wanakosa mawasiliano stahiki wawapo shuleni kutokana na ufinyu wa wataalamu, jambo linaloenda sambamba na wazazi wao kushindwa kuwasiliana nao kikamilifu, hali inayowafanya wakose taarifa muhimu.
“Tuwajengee uelewa wazazi, wajue namna ya kuwapatia huduma stahiki watoto wao, wasiwafiche, wawalete shuleni ili waweze kuelimika,” amesema.
Maneno yake yaliungwa mkono na Stephanie Kitandu ambaye amesema ugumu wanaoupata kuwasiliana na watoto wao wasioweza kuzungumza huwafanya kupata hofu ikiwa wataelewa pindi watakapopelekwa shule.
“Nyumbani tu ukizungumza naye unashindwa kuelewa kama amekusikia vyema na atafanya kile unachokitaka. Unawaza huko shuleni wanakotaka nimpeleke itakuwaje. Hii inafanya usione umuhimu wa kumpeleka kujifunza na kumuacha nyumbani,” amesema Stephanie.
Akiwa ni mama wa mtoto asiyeweza kutembea wala kuzungumza, amesema mara zote humuona kama jukumu lake na huhisi atakapompeleka shuleni hakuna atakayemwangalia sawasawa kama afanyavyo yeye.
“Sidhani kama nitakuwa na amani kwanza, maana kila kitu chake kinahitaji usaidizi wangu. Nilikuwa najaribu kumfundisha hapa hapa nyumbani siku zote, ndiyo maana sasa anaweza kutamka baadhi ya maneno japokuwa kwa umri wake alipaswa kufanya zaidi,” amesema.
Katika kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inagusa kundi la watu wenye ulemavu ipasavyo, Serikali imelenga kuimarisha utoaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi na walimu kwa lengo la kuondoa vikwazo vya kimfumo na kimuundo ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutekeleza yafuatayo:
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2025/2026, ili kufanikisha hilo Serikali itafanya tathmini ya awali ya kubaini hali ya usaidizi uliopo na unaohitajika kwa wanafunzi 1,000 na walimu 200 wenye mahitaji maalum kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalamu.
Hii itajenga uelewa kwa jamii na wadau wa elimu kuhusu suala la elimu jumuishi kwa lengo la kuhamasisha uandikishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Vilevile, itatoa semina za uhamasishaji kuhusu haki na wajibu wa watumishi wenye mahitaji maalumu kwa watumishi 105 kutoka vyuo 35 vya ualimu.
“Pia itawezesha ushiriki wa watumishi 40 katika maadhimisho ya watu wenye ulemavu, itawajengea uwezo maofisa 368 wa elimu maalumu ya msingi na sekondari kuhusu ubainishaji wa awali wa watoto wenye ulemavu kwa lengo la kurahisisha zoezi la upimaji kwa kiwango kinachohitajika,” alisema.
Alisema pia hilo litaenda sambamba na ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vifaa saidizi kwa wakufunzi 105, walimu 103 na walimu tarajali 188 wenye mahitaji maalumu ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.