Hawa wanambana Raheem KMC | Mwanaspoti

WIKI iliyopita, beki wa Kitanzania, Raheem Shomari alitambulishwa kwenye kikosi cha Ghazl El Mahalla ya Ligi Kuu ya Misri kwa mkataba wa miaka mitatu.

Raheem anajiunga na timu hiyo ambayo aliwahi kuichezea Mtanzania mwenzake, Himid Mao, ambaye alicheza kwa kiwango kikubwa.

Kwenye eneo la beki wa kushoto atakalocheza nyota huyo wa zamani wa KMC, kuna nyota wawili ambao wamekuwa wakianza na kuonyesha kiwango kikubwa, Yehia Zakari raia wa Misri na Mghana Hamidu Abdul Fatawi, ambao wote wawili ni msimu wao wa pili kuitumikia timu hiyo.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha nyota hao wote wawili wamekuwa wakicheza kwa kupishana na hakuna mwenye namba moja kwa moja eneo hilo.

Zakari amecheza mechi 18, wakati Fatawi akicheza 19 na hakuna aliyefunga bao wala kutoa asisti. Uchezaji wao wote wawili si wa kupanda juu zaidi kushambulia.

Kwa kiwango alichoonyesha Raheem misimu miwili mfululizo ya Ligi Kuu Bara, akichukua pia tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi, kama atafanya vizuri huenda pia akapewa nafasi kwenye eneo hilo kutokana na aina yake ya uchezaji ya kushambulia na kurudi haraka kukaba.