Akizungumza katika hafla ya tukio la kupanda Mlima Kilimanjaro la Kampeni ya Kili Challenge 2025, katika geti la Machame, Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro jana, wakati wa kuwaaga wapanda mlima 49 na waendesha baiskeli 17, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti wa Masuala ya Uendelevu na Mambo ya Ubia (Afrika), Bw. Simon Shayo alisema kampeni hiyo yenye lengo la kuunganisha juhudi za pamoja kupambana na janga la Ukimwi imekuwa na mafanikio makubwa tokea lipoanzishwa Mwaka 2002 ikifanikiwa kuchangisha Dola za Kimarekani Milion 1 kila mwaka.
“GGM Kili Challenge siyo tu kupanda mlima, ni harakati inayoonyesha nguvu ya umoja na dhamira ya kumaliza VVU/UKIMWI katika kizazi chetu, tunajivunia kuendeleza urithi huu na kuongeza athari chanya mwaka 2025.”
“Fedha zitakazochangwa kupitia tukio hili zitaelekezwa moja kwa moja katika shughuli za kuzuia, kupima, kutibu, kuhudumia na kuelimisha kuhusu VVU/UKIMWI kupitia Kili Challenge Trust Fund, ikinufaisha maelfu ya Watanzania kote nchini”, alisema Bw. Shayo.
Naye Mhandisi Jackson Masaka, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu katika hafla hiyo aliipongeza GGML akisema kampeni hiyo inakwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambayo moja kati ya nguzo zake tatu inasema ‘Uwezo wa Watu na Maendeleo ya Jamii’ hivyo kampeni ya GGM Kili Challenge inagusa nguzo hiyo kwani watu ambao afya zao ni dhaifu, hawawezi kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi hivyo kufanya jamii haiwezi isiwe na maendeleo.
“Natoa pongezi kubwa kwa GGML na TACAIDS ambao ni waanzilishi kampuni hii ya Kili Challenge dhidi ya mapambano ya ukimwi, ambayo kupitia program hii leo tupo hapa kuwaaga mashujaa walijitoa kupanda Mlima Kilimanjaro wenye Mita 5895 na waendesha baiskeli watakaozunguuka mlima huu kwa umbali wa kilomita 480.
“Kama mnavyofahamu nchini yetu bado inaendelea na jitihada za kuzuia maambukizi ya ukimwi Pamoja na athari zake, kwa mujibu wa takwimu za viashiria vya ukimwi mwaka 2022/2023, takrabani watu 1,700 wanaishi na virusi vya ugonjwa huo, huku watu 1,500 ndio wanaotumia dawa za kufubaza ugonjwa huo, aidha takwimu zimeendelea kuonesha kwamba kuna watu 60,000 wanapata maambukizi mapya kila mwaka, hivyo kujitoa kwenu kuna umuhimu sana katika kuhakikisha tunafikia malengo ya kutokomeza ukimwi ifikapo Mwaka 2030”, alisema mhandisi huyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Bw. Yasin Abbas, alipongeza ushirikiano wa muda mrefu na GGML, akisema kampeni ya Kili Challenge 2025 ni mfano bora wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii kupitia Ushirikiano wa Umma na Binafsi (PPP) unavyoweza kuendana na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo, rasilimali zinazopatikana kupitia kampeni hii zinavyoweza kuokoa maisha na kuimarisha jamii.
“Kiwango cha maambukizi kwa takwimu za hivi karibuni kinaonesha kushuka kwa asilimia 4.4, huku wanawake wakiwa na idadi ya maambuki ya asilimia 5.6, wanaume ni asilimia 3.0 maeneo hatarishi zaidi maeneo ya migodi ya madini, maeneo ya uvuvi, madereva wa masafa marefu na vijana wenye umri kuanzia mika 15-24.
“Niwapongeze sana wawakilishi wetu mnaopanda Mlima Kilimanjaro na waendesha baiskeli, maumivu yenu mnayoyapata wakati mnapanda mlima ama kuzunguuka mlima huu, ndio wanayopata wenzetu wanaoishi na ukimwi, jitihada zetu hazitaweza kusahaulika”, alisema Bw. Abbas.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, Kili Challenge imelenga kukusanya Dola za Kimarekani Milioni Moja kila mwaka, na imechangia kwa kiasi kikubwa katika programu za UKIMWI zinazotegemea jamii, hasa katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika.
Kadri wapandaji na waendesha baiskeli wanavyoanza safari yao, ari ya matumaini na dhamira inaendelea kuongezeka, kila hatua ya safari yao mlimani ni sauti ya ujumbe mpana wa kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.