MCHEZO wa kriketi umetinga Kanda ya Ziwa kwa kishindo na kushuhudia Kombaini ya Geita ikishinda kwa wiketi nane dhidi ya Mwanza Kombaini, mwishoni mwa juma.
Michuano hiyo inayojulikana kama TCA Inter-Academy League 2025 – Group 3 ilifanyika jijini Mwanza, Jumamosi na Mwanza Kombaini ndio iliyoanza kubeti na kugota katika mikimbio 53 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 11 kati ya 20.
Geita ilitumia mizunguko tisa kutengeneza mikimbio 58 kushinda, wakipoteza wiketi mbili.
Eligibo Kenedy na Isan Henly walioshinda wiketi tatu kila mmoja na Godfrey Vincent aliyeshinda mbili na kutengeneza mikimbio 20 ndiyo waliochangia kuzama kwa Mwanza katika mchezo huo.
Ulikuwa ni ushindi wa kisasi kwa Geita kwani mchezo wa kwanza, Mwanza ilishinda pia kwa wiketi nane.
Katika mchezo huo, Geita ndiyo iliyoanza kubeti na kufikisha mikimbio 50, huku ikipoteza wiketi tisa baada ya mizunguko yote 20.
Ikitumia mizunguko saba kati ya 20, Mwanza ilijibu vyema kwa kupiga mikimbio 51 huku ikipoteza wiketi mbili na kushinda kwa wiketi nane.
Vinara wa ushindi wa Mwanza walikuwa ni Joshua Ibrahim aliyepiga mikimbio 15 na kushinda wiketi moja, Pascal Pastory aliyetengeneza mikimbio 12 na kushinda wiketi moja na Aizack John mikimbio 10 na kushinda wiketi moja.