Madaktari wataja kipimo sahihi kubaini, kuitibu PID

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na utitiri wa dawa za kutibu tatizo la maambukizi ya bakteria katika mfumo wa uzazi wa mwanamke ‘PID’ wataalamu wa afya nchini wametaja kipimo sahihi cha kubaini tatizo hilo na kulitibu, mchakato unaojumuisha kuotesha viini vya maradhi maabara.

Wamesema bila kipimo hicho ni ngumu kuitibu, kwani asilimia 85 ya PID husababishwa na vimelea wanaoambukiza magonjwa ya zinaa, hasa ni bakteria jamii ya Neisseria Gonorrhoeae na Chlamydia trachomatis na asilimia inayobaki husababishwa na wadudu wengine.

Akizungumza na Mwananchi, daktari kutoka kitengo cha mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT Justin Nkulu amesema kwa kuwa bakteria hao ndiyo husababisha PID ni lazima kumjua bakteria halisi aliye chanzo cha tatizo ili ujue namna ya kutibu.

“Ili umjue lazima kufanya kipimo. Tutachukua uchafu au majimaji ya ukeni tunaotesha maabara na kufanya ‘culture’ (kipimo cha kuotesha vimelea maabara) itatuambia ni mdudu aina gani aliyesababisha maambukizi.

“Tukishamjua, tutajua dawa gani itakayofaa kuua yule bakteria. Hivyo, tunashauri mama asimeze dawa hovyo, bila ushauri wa daktari kwa sababu katika kumeza antibaotiki mara kwa mara bila ushauri wa daktari anajitengenezea usugu wa dawa,” amesema.

Amesema wakati wa kubaini pia hufahamu iwapo PID aliyonayo mama ni ya muda mrefu na ya kujirudiarudia au mfupi hivyo matibabu pia hutofautiana.

Daktari bingwa wa magonjwa na kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge amesema kuna vipimo vya aina nne kubaini PID.

“Kuna kipimo cha Utrasound inatusaidia kubaini majimaji au usaha ndani, pia kutumia uteute unaotoka kwa mama kama uchafu tunafanya kipimo cha ‘culture’ hii inatusaidia kumgundua mdudu gani alisababisha hiyo PID, kuna kipimo cha damu, kuna raparascopic tunachukua sampuli na kupima lakini kwa maeneo ya vijijini daktari anapima kwa mikono,” amesema Dk Mkeyenge.

Dk Nkulu amesema bakteria hao huingia sehemu za uke kushambulia kizazi, na kukifanya kiongezeka ukubwa na kuvimba, kisha huanza kutengeneza dalili zake hivyo ni daktari pekee mwenye uwezo wa kuibaini PID.

“PID siku hizi ni tatizo kubwa na madhara yake ni kutoshika ujauzito, wale bakteria wanaosababisha PID wanashambulia mlango wa kizazi, mirija ya uzazi na mayai kinachotokea watatengeneza vidonda kwenye mirija, vikipona vinatengeneza makovu kisha mirija inaziba,” amesema.

Dk Nkulu amesema mirija ikiziba mbegu za mwanamume na yai haviwezi kupata nafasi ya kukutana, hivyo huyu mwanamke hatafanikiwa kushika ujauzito, tatizo ambalo ni kubwa kwa kinamama.

“Kinamama wengi sasa hivi tunakutana nao, hawana uwezo wa kubeba ujauzito. Unakuta mrija umeshaharibika, hauwezi tena kutibika huyu tunamshauri ashike mimba kwa njia ya upandikizaji gharama zake ni kubwa zaidi ya milioni 15 mpaka 20.”

Amesisitiza kuwa, mwanamke anapoona dalili za maumivu chini ya kitovu, wakati wa tendo, hedhi kuchelewa au kuwa na mvurugiko na tatizo la kushika ujauzito usitumie dawa bila kufanya vipimo sahihi na ushauri wa kitaalamu.

“Ukijitibu mwenyewe utapata tatizo la usugu wa bakteria dhidi ya dawa na tatizo litaendelea kukomaa kisha utatengeneza nafasi mirija kuziba.”

Hata hivyo amesema PID isipotibiwa kwa wakati, kuna uwekezano mkubwa wa kutengeneza mazingira ya kirusi cha HPV kuleta athari kwa kupata nafasi ya kupenya kwa sababu tayari mazingira yameshachochewa.

Dk Nkulu ametaja dalili za PID ni kuumwa chini ya kitovu, maumivu yanayoweza kusambaa mpaka kiunoni, maumivu wakati wa kujamiiana, hedhi kuvurugika, kutokwa na uchafu sehemu za siri wenye harufu kali na unaoambatana na miwasho au hapana.

Kwa mujibu wa Dk Nkulu amesema PID kwa sasa inawkauta zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa miaka 15 mpaka 25.

Amesema wapenzi wanapofanya tendo la ndoa bila kutumia kinga wanakuwa hatarini zaidi kupata PID hasa matumizi ya P2 na wanawake wanaotumia kitanzi pia wapo hatarini.

“Hili ni kundi ambalo linahamasika na ngono na hawajawa na elimu ya kutosha namna gani ya kujikinga wanapokwenda kujamiiana. Mara nyingi pia ni kwa kinamama wenye wapenzi wengi.

“Mwanamke anapata PID kutoka kwa mwanamume ila mwanamume hapati hana kizazi yeye anapelekwa kwa mwanamke mwingine. Kama mwanamke ana PID atamwambukiza mwanamume naye atapeleka kwa mwanamke mwingine.”

Ametaja visababishi vingine kuwa ni kuharibika kwa mimba, kusafishwa mara kwa mara na matumizi ya kemikali ukeni.