Wazee walalama kutopewa kipaumbele kwenye huduma za kijamii

Unguja. Wazee na wastaafu visiwani Zanzibar wamesema wanakumbana na changamoto ya ucheleweshwaji wa huduma ikiwamo kwenye usafiri wa umma, hospitali na benki.

Wamewasilisha malalamiko hayo kupitia Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (Juwaza), leo Jumapili Julai 20, 2025 kwenye kongamano la siku ya kupinga udhalilishaji kwa wazee duniani lililofanyika Sebleni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Akizungumza kwenye kongamano hilo Katibu wa jumuiya hiyo, Salama Kombo Ahmed amesema wazee wengi wanapofika katika maeneo hayo huchuka muda mrefu kusubiri kuhudumiwa, bila kupewa kipaumbele jambo ambalo sio sawa kwao.

“Wazee wengi wanakaa kwa muda mrefu kusubiri huduma za kijamii kwenye maeneo kama hospitali, benki na kwenye usafiri wa umma. Kwenye maeneo hayo hatupewi kipaumbele, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwetu kiafya na kiakili,” amesema Salama.

Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wazee wanaofanyiwa udhalilishaji wasikae kimya badala yake watoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hassan Ibrahim amesema Serikali itaendelea kuwatunza, kuwalinda na kuwapa heshima wazee  kwa kutambua kuwa wao ni hazina ya Taifa kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa jamii.

Mkurugenzi huyo amesema wizara itafuatilia changamoto zilizowasilishwa katika kongamano hilo kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka.

“Licha ya changamoto hizo, Zanzibar ni miongoni mwa maeneo machache duniani yanayotoa kipaumbele kwa ustawi wa wazee kwa kuwapatia huduma stahiki na heshima wanazostahiki,” amesema Hassan.

Pia, amebainisha kuwa zaidi ya Sh300 milioni zimetengwa kuimarisha mabaraza ya wazee kwa lengo la kuwapa fursa ya kupaza sauti na kusimamia haki zao katika jamii.

Mkurugenzi huyo, amewaasa vijana kuwatunza na kuwaheshimu wazee, akiwataka kuepuka vitendo vya kuwadhalilisha ikiwemo kuwatolea lugha chafu, kuwafukuza majumbani, na kuwaita wachawi kwa sababu vitendo hivyo vinautweza utu wao.

Kwa upande wake,  Mjumbe wa Baraza Mkoa wa Mjini Magharibi, Mzee Issa Kidali amepongeza juhudi za Serikali na kuomba kuwepo kwa mwakilishi maalumu wa wazee katika Baraza la Wawakilishi ili kusimamia haki zao katika mamlaka zinazotoa maamuzi.