Unguja. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohammed amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua ya kuhakikisha taarifa binafsi zinalindwa na sheria inachukua mkondo wake pindi haki za watu zinapovunjwa.
Dk Khalid ametoa kauli hiyo Julai 20, 2025 wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa maofisa habari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), na waandishi wa Habari yaliyoandaliwa na Tume ya Ulizi wa Taarifa Binafsi (PDPC).
“Tunaishi kwenye dunia ambayo taarifa binafsi kwa sasa zinasambazwa kwa urahisi kutokana na kukua wa teknolojia, kwa mantiki hiyo suala la kulinda taarifa hizo haliwezi kupuuzwa, faragha ni haki ya kila mtu ni wajibu wetu kuhakikisha haki hiyo inalindwa,” amesema.
Amesema taarifa binafsi. zina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya kila mtu iwe ni jina, anuani, namba ya simu, taarifa za afya au nyinginezo nyeti.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano kupitia ibara ya 16 inasisitiza kuwa faragha ni haki ya msingi ya kila Mtanzania.
Amesema uelewa wa dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi ni msingi muhimu katika zama za sasa za kidijitali na kutokuelewa kwa kina dhana hii kunaleta hatari ya kukumbwa na migogoro ya kisheria kama ambayo imeshuhudiwa katika baadhi ya mataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk Emmanuel Mkilia amesema vyombo vya habari vina jukumu la kulinda taarifa binafsi kwa mujibu wa sheria, ili zisitumike vibaya.
Amesema sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi namba 11 ya mwaka 2022 inalinda haki hiyo, kwa lengo la kuhakikisha kuwa taarifa za watu zinatumika kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji.
Ameongeza kuwa sheria hiyo pia imetungwa ili kukidhi matakwa ya kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ibara ya 16, na ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ibara ya 15.
“Taarifa binafsi zinaweza kutumika vibaya na kusababisha wizi wa utambulisho, ambao madhara yake ni pamoja na udanganyifu wa kifedha na hata unyanyapaa,” amesema.
“Nafasi ya waandishi wa habari katika zana ya ulinzi wa taarifa binafsi ni wadau muhimu kuhakikisha faragha zinalindwa huku wakihakikisha jamii inapata habari sahihi na zenye manufaa,” amesema
Kwa upande wake wakili kutoka PDPC, Humphrey Mtuy amesema kutoa taarifa binafsi bila ridhaa ya muhusika ni kosa na mtu akibainika, anaweza kutozwa faini ya kati ya Sh100,000 hadi Sh10 milioni au kifungo cha miaka mitano hadi 10 au vyote kwa pamoja.
Ofisa mwingine kutoka Tume hiyo, Innocent Mungy, amesema bila kuathiri sheria za habari, vyombo vya habari vina wajibu mkubwa kuhakikisha vinalinda taarifa binafsi.
“Sheria ipo lakini mabadiliko ya tabia yanahitajika zaidi, kwani kuna madhara makubwa pindi taarifa binafsi za mtu zinapovuja,” amesema
Naye Mkurugenzi wa usajili na uzingatiaji wa tume hiyo, Stephen Wangwe amesema kuna misingi minane ya ulinzi wa taarifa binafsi ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki za mhusika, taarifa kuwa sahihi na kuendana na wakati.