Dodoma. Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Kata 41 za Wilaya ya Dodoma wameishawasili katika Ukumbi wa Chuo Cha Mipango kwa ajili ya uchaguzi.
Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) wanakutana kufanya uchaguzi huo leo Jumapili Julai 20, 2025 ambao unahusu madiwani wa viti maalumu.
Jana Jumamosi Julai 19, 2025 CCM kilitangaza kuwa Julai 28, 2025 itakuwa siku ya mchujo huku kikisitisha mchakato wa mchujo kwa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ulipangwa kufanyika jana.
Hata hivyo Katibu wa Itikadi, Siasa, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho Amos Makalla alieleza kuwa mchakato wa uchaguzi kura za madiwani wa viti maalumu unaendelea kama kawaida.
Kwa Wilaya ya Dodoma wagombea zaidi ya 80 waliomba kuteuliwa kwenye kinyang’anyiro hicho lakini CCM kimerudisha majina 24 ambapo watachaguliwa 12.
Ulinzi katika eneo la kuzunguka majengo ya chuo ni wa kiwango cha juu huku baadhi ya walinzi wakionekana ndani ya sare za chama hicho.
Mbali na kulinda maeneo ya lango la kuingilia na nje, baadhi ya watu ambao haikujulikana mara moja wanatoka taasisi zipi, walikuwa wakiyafuata magari ya wajumbe kila yaliposimama.
Wagombea wote wa nafasi hiyo walifika ukumbi mapema na walitakiwa kuingia ndani ya ukumbi ili kuchukua namba za utambulisho lakini ikawa walipoingia milango ilifungwa.
Chanzo cha kufungwa milango kilitajwa kama sehemu au mbinu za kukomesha vitendo vya rushwa kutokana kwa wagombea.
Taarifa zinasema kuwa kila mgombea aliombwa kuzima simu yake na kukabidhi mikoba anapoingia.