Geita. Wajumbe 3,000 wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Wilaya ya Geita leo wameshiriki kuwapigia kura wanachama 20, watakaowakilisha wanawake kwenye mabaraza ya madiwani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Manispaa ya Geita.
Uchaguzi huo unaofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Nyankumbu, unahusisha wagombea 46 kutoka tarafa tano za wilaya hiyo, ambapo ni wanachama 20 pekee watakaopata nafasi ya kuingia kwenye orodha ya madiwani wa viti maalumu kupitia CCM.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Hashim Komba amesema mchakato huo unalenga kumpata mwakilishi wa wanawake serikalini na si mshindi au aliyeshindwa, akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kwa uwazi, uhuru na haki.
“Hatujaja kumtafuta mshindi kwa kuwa hakuna anayeshindwa. Tunatafuta mwakilishi atakayesimamia masilahi ya wanawake kwenye vyombo vya maamuzi. Uchaguzi huu utakuwa wa haki na wazi,” amesema Komba.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Michael Msuya amesema maandalizi yamekamilika na wajumbe wote 3,000 walioorodheshwa wanatarajiwa kupiga kura kwa kufuata kanuni na taratibu za chama.
“Tumejipanga kuhakikisha kila kitu kinaenda kwa utaratibu. Kwa wajumbe watakaopatwa na msisimko mkubwa, tumeandaa glucose na maji kuhakikisha hali inakuwa shwari. Niwaombe sana wajumbe wasiharibu kura, tumalize hili kwa umoja wetu,” amesema Msuya.
Wilaya ya Geita ina jumla ya majimbo manne ya uchaguzi ambayo ni Geita Mji, Geita, Busanda na Katoro, pamoja na kata 50 zinazoshiriki uchaguzi huo.
Huku kampeni za ndani ya ukumbi zikiendelea kwa wagombea kuomba kura, msimamizi wa uchaguzi ametoa agizo kwa washiriki wasiokuwa wapigakura, wakiwemo waandishi wa habari, kuondoka ndani ya ukumbi ili kutoa nafasi kwa wajumbe kufanya maamuzi yao kwa utulivu.