Rufaa ilivyomnusuru kifungo cha maisha jela kwa ubakaji, ulawiti

Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru Bahati Anyandile, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya kumbaka na kumlawiti mtoto wa mpangaji mwenzake  aliyekuwa na miaka minne.

Matukio hayo yalidaiwa kutokea kwa tarehe isiyojulikana Aprili 2021. Anyandile alifanya vitendo hivyo mara nane kwa nyakati tofauti maeneo ya chumbani kwake, chooni na bafuni.

Mama wa mwathirika wa tukio hilo ambaye katika kesi ya msingi alikuwa shahidi wa pili, aliieleza Mahakama kuwa alikuwa akimkagua mtoto wake mara kwa mara sehemu za siri.

Hukumu iliyomuachia huru Anyandile ilitolewa Julai, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Dk Mary Levira, Sam Rumanyika na Agnes Mgeyekwa.

Kupitia nakala ya hukumu iliyowekewa kwenye mtandao wa Mahakama, majaji hao wamesema ushahidi wa upande wa mashtaka haukuwa wa kuaminika.

Awali, mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Anyandile alisomewa mashtaka ya ubakaji na ulawiti kinyume na vifungu vya 130 (1), (2) (e), 131 (1) na (3), na 154 (1) (a) vya Kanuni ya Adhabu.

Awali, alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kila kosa, adhabu zilizoamriwa kutekelezwa kwa wakati mmoja.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa Aprili, 2021 eneo la Ngerengere Mkoa wa Morogoro, mrufani alimbaka mtoto huyo.

Kosa la pili alidaiwa kumlawiti mtoto huyo.

Ushahidi wa Jamhuri ulieleza kuwa, mrufani na familia ya mwathirika wa tukio hilo waliishi kama wapangaji wenza.

Ilidaiwa mahakamani kuwa, shahidi wa kwanza (mwathirika wa tukio hilo) hakwenda shule kwa sababu alikuwa anaumwa na wazazi wake walikuwa mbali na nyumbani.

Ilielezwa kuwa, Anyandile alitumia nafasi hiyo ya kutokuwepo kwa wazazi wa mtoto huyo kumbaka na kumlawiti na kumwambia asiseme jambo hilo kwa mtu yeyote.

Akitoa ushahidi mahakamani hapo, mama wa mtoto huyo alidai kuwa, alikuwa akichunguza mara kwa mara sehemu za siri za mtoto wake na kila kitu kilikuwa sawa.

Alieleza kuwa, Aprili 6, 2021 alimkagua mwanaye baada ya kugundua hayuko sawa na akabaini sehemu za siri na haja kubwa hazikuwa sawa kwa madai zilikuwa zimelegea, akaamua kumshirikisha mumewe juu ya hali hiyo.

Shahidi huyo alieleza kuwa, baada ya kumdadisi mtoto wake ni nani aliyemfanyia kitendo kibaya, ndipo alimtaja Anyandile.

Shahidi wa tatu ambaye ni daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Jamila Masola aliiambia Mahakama kuwa, alimchunguza mtoto huyo Aprili 12, 2021 na kuthibitisha sehemu za siri zilikuwa zimelegea na alibaini ameingiziwa kitu butu kwenye sehemu zake za siri na alikuwa na michubuko.

Katika utetezi wake, Anyandile alikana mashtaka hayo na kudai kuwa, Aprili 2021 hakuwa Ngerengere kama inavyodaiwa bali alikuwa akiendelea na shughuli zake za udereva katika Kampuni ya Yapi Merkez nje ya Ngerengere.

Mahakama hiyo ya chini ilishawishika pasipo shaka kwamba, mtoto huyo alibakwa na kulawitiwa na mrufani huyo, hivyo kumtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Hii ni rufaa yake ya pili, rufaa ya kwanza aliikata Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro; Oktoba 31, 2023 Mahakama hiyo ilitupilia mbali.

Katika rufaa ya pili iliyosikilizwa na Mahakama hiyo ya juu nchini katika vikao vyake vilivyoketi Morogoro, Anyandile alikuwa na sababu tisa za rufaa  ikiwamo kesi dhidi yake kutothibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Anyandile alikuwa mwenyewe bila uwakilishi wa wakili huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na mawakili watatu.

Mrufani huyo aliieleza Mahakama kuwa, katika makosa ya kujamiiana katika kesi dhidi yake haikuelezwa ni mara ngapi mtoto huyo aliingiliwa kingono.

Alieleza kuwa, haijulikani kama ni mara nane kama ilivyodaiwa awali kwa madai kuwa mwathirika alidai hakumbuki ni mara ngapi alinyanyaswa kingono.

Mrufani huyo alidai kuwa, dosari hizo na ushahidi wa mama wa mtoto, ulifanya mashtaka kutothibitishwa na kuomba Mahakama ikubali rufaa yake na kumuachia huru.

Upande wa mjibu rufaa, ulieleza mashtakiwa dhidi ya Anyandile, yalithibitika hadi mwisho na suala la tofauti kati ya shtaka na ushahidi halikutokea.

Alidai kuwa, mwathirika wa matukio hayo alikuwa mtoto wa miaka minne na ushahidi wake ulirekodiwa baada ya kuahidi mahakamani kusema ukweli.

“Ushahidi wa shahidi huyo wa kwanza ulikuwa dhahiri, alisema mrufani alimlawiti mara nane katika chumba chake cha kulala, chooni na wakati mwingine bafuni, ushahidi wa mtoto mara zote huwa hautiliwi shaka,” alisema upande wa mjibu rufaa.

Zaidi ya hayo, ilielezwa kuwa, mtoto huyo alimtaja mrufani ndiye aliyefanya vitendo hivyo na kuhusu ushahidi wa mama wa mtoto, uliunga mkono ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo.

Aidha, iliielekeza Mahakama katika kielelezo cha pili ambacho ni ripoti ya daktari iliyoonesha kuwa, sehemu za siri za mwathirika wa tukio hilo zililegea, zilikuwa na michubuko na zilionesha kupenya kwa kitu butu, hivyo ushahidi ulikuwa wa kuaminika.

Baada ya kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili, jopo la majaji hao lilisema linaangalia iwapo ushahidi uliotolewa ulithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Jaji Rumanyika alisema ili kuthibitisha makosa hayo, masuala matatu yatakayoangaliwa ni umri wa mwathiriwa, kutendeka kwa vitendo hivyo na iwapo mrufani ndiye mhusika wa makosa hayo.

Alisema ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo kuwa, mrufani ndiye alimfanyia vitendo hivyo bado vinaacha maswali mengi.

Jaji alisema mwathirika alidai kufanyiwa vitendo hivyo mara nane kwa muda tofauti.

Alisema licha ya Mahakama kutambua kuwa, makosa ya ngono ushahidi mzuri na wa kweli  hutoka kwa mwathirika, lakini siyo lazima na katika kesi hiyo, ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo ulihitaji kuthibitishwa pasina kuacha shaka.

“Hata hivyo, mama wa mtoto hakuweza kuithibitishia Mahakama juu ya hilo, lakini pia mazingira ya kesi na ushahidi wake kwamba alipochunguza sehemu za siri za mwathiriwa aligundua kwamba kitu butu kilipenya kwenye sehemu za siri za mwathirika, unatiliwa shaka,” alisema Jaji.

Alisema wanatambua kwamba, mwathiriwa alikuwa mtoto wa umri mdogo ambaye ushahidi wake unahitaji kuchukuliwa kwa uangalifu, lakini ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili unaacha maswali mengi.

Miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na mwathirika alikuwa mtoto wa umri mdogo ambaye asingeweza kukumbuka maelezo yote ya kesi, kama vile ni lini hasa madai ya makosa mawili yalifanywa.

Nyingine ni ushahidi wake kutofautiana na wa shahidi wa pili, na ndiyo sababu ya majaji hao kujiuliza iwapo shahidi huyo alikuwa akichunguza sehemu za siri za mtoto wake mara kwa mara kama alivyodai, kwa nini alichelewa kugundua kwamba mtoto wake alibakwa na kulawitiwa.

“Kwa kukosekana kwa ushahidi wowote thabiti wa kuthibitisha ushahidi wa shahidi wa pili ambao pia, kwa asili yake hauwezi kuthibitisha ule wa shahidi wa kwanza tunashikilia kwamba kesi ya mashtaka haikuthibitishwa,” alisema.

Jaji huyo alisema ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo kuwa mrufani alimfanyia vitendo hivyo mara nane katika sehemu tofauti ikiwemo bafuni, chooni na chumbani, ulikuwa ushahidi ambao hauendani na kiwango cha uwezo wa kumbukumbu kwa umri wa mtoto huyo.

“Sasa kwa kuwa, kwa sababu zilizotangulia, ushahidi wa mashahidi wawili muhimu uliotajwa haufai kitu, tunakubali rufaa na kufuta hudumu iliyotolewa kwa mrufani na tunaamuru aachiliwe mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali,” alihitimisha Jaji huyo.