Conte, Ecua wapelekwa Misri | Mwanaspoti

MABOSI wa Yanga wamebadilisha gia angani mara baada ya kumpa ajira kocha mpya Romain Folz atakayetambulishwa wiki hii, ambaye ametaka mastaa wa timu hiyo wakiwamo wapya kina Mousa Conte, Mohamed Doumbia na Celestin Ecua kambini Misri kwa kazi maalumu.

Inadaiwa kuwa, kocha Folz ameambiwa na mabosi wa Yanga kwamba kulikuwa na hesabu za timu hiyo kwenda Namibia, Rwanda au Afrika Kusini kwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya kisha jamaa akaja na akili mpya.

Mwanaspoti linafahamu kuwa; “Kocha huyo amewaagiza mabosi wa Yanga kwamba, timu yake itakwenda Rwanda pekee kwenye mchezo maalum ambao alishindwa kuupangua kwa kuwa ni makubaliano ya pande mbili kati ya Rayon Sport na Yanga.

“Maana yake ni hivi, huenda Yanga itakuwa Rwanda Agosti 15 ambapo baada ya hapo kocha huyo amewataka mastaa wote wapya wakiwemo Celestin Ecua na Moussa Bala Conte na wale za zamani kuwa safarini kuelekea Misri ambako anataka kambi yao iwekwe huko.”

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba; “Hesabu za kocha huyo zilizokubaliwa na mabosi wa timu hiyo ni kwamba wakati huo nchini Misri kutakuwa na utulivu mkubwa kwa kuwa timu nyingi zitakuwa zimekwenda kwenye kambi mbali  zitasalia timu za kawaida ambazo ndio wanazozitaka.”

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Yanga kwenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya Misri, ambapo mara ya mwisho kwa nchi za Afrika Kaskazini, iliwahi kutua Morocco ilipoweka kambi Jiji la Marrakech miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mabosi wa Yanga, bado hawajajua ni mji gani ambako kambi hiyo itawekwa ambapo mchakato wa kukamilisha hilo unaendelea.

“Tumeshabadilisha timu ina kocha tayari na amekuja na mapendekezo yake, kule Namibia na Afrika Kusini hakutaendeka tena kocha amekataa na ametuagiza tutafute sehemu ya kwenda lakini iwe ndani ya Misri,” alisema kiongozi huyo.

“Ametupa sababu na tumezielewa na yanafanyiwa kazi haraka nadhani timu ikiondoka hapa kwenda Rwanda kwenye ile mechi ya Rayon haitarudi hapa tena iteelekea huko. Anataka wachezaji wote wa timu yake wawepo kwenye safari hiyo kasoro hawa ambao wako kwenye mashindano ya CHAN ambao nao itategemea na hatua watakayofikia.”

Folz ametua Yanga kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Miloud Hamdi aliyetua Ismailia ya Misri mara baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) msimu uliomlizika hivi karibuni.