Mabosi Simba washtuka! | Mwanaspoti

MABOSI wa Simba wameshtuka. Baada ya kushindwa kumnasa Balla Mousa Conte, kisha kumpoteza beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ anayedaiwa kusajiliwa Yanga kwa mkataba wa miaka miwili, kumewafanya wazinduke na kuanza kufanya mambo yao kimyakimya.

Simba iliyoanza kumfukuzia Bella Conte, ilijikuta ikipigwa bao wikiendi iliyopita baada ya Yanga kumtambulisha na jana watani wao hao walikuwa mbioni kumpa mkataba mpya Tshabalala, beki na aliyekuwa mchezaji mwandamizi wa timu hiyo akiitumikia miaka 11 tangu 2014.

Ikihofia kuzidi kuubomoa ukuta wa timu hiyo iliyoondokewa na wachezaji saba wanaocheza eneo la ulinzi akiwamo kipa Aishi Manula, mabeki Kelvin Kijili, Tshabalala, Hussein Kaze na viungo Fabrice Ngoma, Debora Mavambo na Augustine Okejepha, imeamua kumkomlia Shomary Kapombe.

Mabosi wa Simba imeamua kumuita haraka mezani, Kapombe aliyemaliza mkataba kama ilivyokuwa kwa Tshabalala, ili kufanya mazungumzo ya kumpa mkataba mpya wa kuendelea kuwepo katika kikosi hicho msimu ujao kama ripoti ya kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids inavyotaka.

Chanzo cha ndani kinasema kitendo cha kuondoka kwa aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Tshabalala aliyesaini mkataba wa miaka miwili Yanga, uongozi hautaki kumpoteza Kapombe atakayebakia kama mchezaji mwandamizi ndani ya kikosi hicho kitakachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Mazungumzo ya kumuongezea Kapombe mkataba wa miaka miwili yameanza kufanyika na yana muelekeo mzuri, kwa asilimia kubwa tunaamini ataendelea kuwa sehemu ya kikosi kama ripoti ya kocha Fadlu ilivyotaka,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kapombe ameitumikia Simba kwa mafanikio kwa muda mrefu tunamchukulia kama mchezaji kiongozi dhidi ya wengine na ikiwezekana kwa baadaye aje kuinufaisha zaidi Simba kama ilivyokuwa kwa kina Mussa Mgosi, kocha wa Simba Queens, Selemani Matola aliye kocha msaidizi wa muda mrefu wa Simba.”

Msimu uliyopita Kapombe alifunga mabao matatu, asisti tatu, msimu wa nyuma yake 2023/24 alimaliza na asisti nne pia aliwahi kuwa MVP wa Ligi Kuu mwaka 2016.

Mbali na hilo msimu wa 2015/16  Kapombe aliweka rekodi ya kufunga mabao manane Ligi Kuu, akifunga moja Azam FC ikishinda mabao 2-1  dhidi ya Coastal Union, dhidi ya Ndanda FC bao 0-1, dhidi ya Toto Africans mabao mawili Azam ikishinda mabao 5-0, dhidi ya Mgambo Shooting 2-0 dhidi ya Stand United bao 0-1 dhidi ya Kagera moja Azam ikishinda mabao 2-0. 

Kuhusiana na maamuzi ya Simba kumbakiza Kapombe, staa wa zamani wa timu hiyo, Amir Maftah alisema: “Kikosi kinapokuwa na wachezaji wapya na waandamizi kinakuwa imara zaidi, Kapombe kaitumikia Simba kwa muda mrefu, hivyo anaweza akawa kiongozi mzuri dhidi ya wengine.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa klabu hiyo, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema: “Simba wakimbakiza Kapombe watakuwa wamefanya kitu sahihi,baada ya kuondoka kwa Tshabalala lazima abakie kama mchezaji mwandamizi.”