MABOSI wa Simba baada ya kutafakari kwa kina na hasa baada ya kuondokewa na mabeki wawili wa kushoto, wameamua kufanya jambo moja ili kujiweka salama kwa msimu ujao kwa kumrudia beki mmoja wa maana anayekipiga pale Al Hilal ya Sudan.
Simba imeondokewa na mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Valentin Nouma waliokuwa wakipokeza eneo la kushoto, huku Kelvin Kijili aliyekuwa akicheza kulia sambamba na Hussein Kazi anayemudu beki ya kati ni wachezaji ambao hawakuwa kikosi cha msimu ujao.
Kutoka na hali hiyo, mabosi wa klabu hiyo wameamua kurudi mezani kuzungumza na beki kushoto wa Al Hilal ya Sudan, Khadim Diaw (26), ili kuzipa pengo la Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyejiunga na Yanga kwa ajili ya msimu ujao.
Awali uongozi wa Simba ulizungumza na mchezaji huyo kisha ukampotezea, kwani haukutegemea suala la Tshabalala lingefikia kikomo kuichezea klabu hiyo.
Baada ya Tshabalala kuaga rasmi akitajwa kujiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili, Simba imerejea kwa nguvu ili kuhakikisha Diaw anakuwa mbadala wake.
Chanzo cha ndani kutoka klabu hiyo kilisema: “Ni beki mzuri tulimuona katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) ambapo alicheza mechi 12 na alikuwa na kadi za njano mbili.
“Ni beki mwenye kasi ya kupanda na kushuka kukaba, ana uwezo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi, tukifanikiwa kumsainisha basi tutakuwa tumempata mchezaji mzuri, ila haimanishi hatuheshimu mchango wa Tshabalala, alichokifanya Simba kitasalia kuwa heshima na tunamtakia kila lakheri katika maisha mapya aendako.”
Chanzo hicho kilieleza nje na kuondoka kwa Tshabalala pia kuachana beki wa kigeni Valentin Nouma rai wa Burkina Faso ambaye aliyesajiliwa msimu ulioisha akitokea FC Lupopo ya DR Congo, kunatilia mkazo kuhitaji huduma ya Diaw.
“Lengo la kocha Faldu anahitaji wachezaji wenye viwango vya juu watakaisaidia timu kuwania ubingwa wa Ligi Kuu na CAF, ndiyo maana uongozi tunajitahidi kwa kila linalowezekana kuhakikisha tunatimiza matakwa yake,” kilisema chanzo hicho.