Tshabalala Done Deal! | Mwanaspoti

HATA kabla saa 24 kutimia tangu alipowaaga mashabiki na wapenzi wa Simba, aliyekuwa beki wa kushoto na nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amehamia mtaa wa pili.

Beki huyo wa kimataifa anayeitumikia pia timu ya taifa, juzi aliaga rasmi Msimbazi baada ya kuitumikia kwa miaka 11, ikiwa ni saa chache tangu arejee nchini kutoka Misri alipokuwa na Taifa Stars kambini.

Taarifa ni kwamba Tshabalala kwa sasa ni Mwananchi baada ya jana Jumapili kusainishwa mkataba wa miaka miwili na kuungana nyota kadhaa waliowahi kuhama mtaa kutoka Simba kwenda Simba au kutoka Simba kutua Yanga ikiwa ni baada ya kuitumikia kwa miaka 11 Wekundu wa Msimbazi aliomaliza nao mkataba.

Kama hujui, jana Jumapili pale Yanga kulikuwa na tukio moja tu kubwa la kupambana kumalizana na Tshabalala baada ya ofa iliyomuwekea mezani kuizidi kimo Wekundu ambao walishindwa kumuongezea mkataba mpya na kuacha hadi uishe na kutoa nafasi kwa Yanga kuwapiga bao.

Tshabalala aliyeichezea Simba kwa miaka 11 akisajiliwa akitokewa Kagera Sugar 2014, juzi jioni aliwaaga rasmi viongozi, makocha na mashabiki wa timu hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Hatua ya Tshabalala kuaga ni kufuatia Simba kushindwa kumalizana naye, baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu uliomalizika.

Simba ilikumbana na vigingi viwili kwenye kuokoa nahodha wao huyo kuwakimbia, ambapo kwanza ilikuwa ikitakiwa kupambana kuizidi ofa kubwa aliyowekewa na Yanga.

Yanga ilimuwekea Tshabalala mkataba wenye mambo mazuri mengi yakiwemo dau zuri la usajili (japo halijaweka wazi, ila inaelezwa ni zaidi ya Sh 300 milioni), mshahara ambao ni mara mbili ya ule aliokuwa akiupata Simba lakini uhakika wa nafasi kikosi cha kwanza, kama haitoshi haki zake za matangazo binafsi.

Kigingi cha pili kwa Simba kilikuwa ni mahusiano kati ya baadhi ya vigogo wa timu hiyo na wasimamizi wa beki huyo wa kushoto ambapo Mwanaspoti linafahamu kuwa Wekundu hao walitakiwa kulipa kiasi cha Sh 28 milioni kwa Menejimenti ya mchezaji huyo ikiwa ni deni la kamisheni wakati mchezaji anaongeza mkataba uliokwisha.

Licha ya kwamba kiasi hicho si kikubwa kwa Simba, utata ulikuja kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ amewajibu wasimamizi wa mchezaji huyo kuwa hatotoa mara mbili fedha hizo kwa kuwa alishazitoa na kuzusha utata ndani ya mazungumzo hayo na kushindwa kupatikana kwa muafaka.

Yanga haikuwa na hesabu sana na Tshabalala, lakini kufuatia ripoti mbili za makocha walioifundisha timu hiyo msimu uliomalizika, zilionyesha zinahitaji beki mwenye muendelezo wa kiwango kama Tshabalala.

Ripoti hizo zilienda mbali zaidi zikiutaja upande wa beki wa kushoto ndio umekuwa njia kuu ya wapinzani kutengeneza mabao na hata ushindi. Yanga ya msimu uliopita ilikuwa na mabeki wa kushoto, Chadrack Boka na Nickson Kibabage waliokuwa wakipigwa tafu wakati mwingine na Kibwana Shomary na Denis Nkane pamoja Israel Mwenda.

Kufuatia kususua kwa mazungumzo baina ya beki huyo na Simba, iliifanya Yanga itue kibabe kwa wasimamizi wa mchezaji huyo na kuwapa ofa yao huku ikiwataka wasivuke Julai 20 kabla ya kuwapa majibu ya kipi wameamua.

Wakati Simba ikiendelea kuwa kimya, Tshabalala na wasimamizi wake, hawakuwa na chaguo lingine zaidi ya kuaga ili waiwahi ofa ya Yanga ambayo ndio ilikuwa kimbilio pekee na yenye manufaa.

Familia ya beki huyo nayo ilikuwa na wasiwasi haikuamini kama Simba imekaa kimya namna hiyo ambapo ililazimika kuokoa jahazi kwa kuzungumza nao, lakini ikakutana na ugumu kuendelea kuwarudisha mabosi wa Wekundu hao mezani kisha kukubaliana na maamuzi yake.

Yanga jana ilikuwa inapambana kutafuta upenyo tu beki huyo asaini mkataba wa miwili, akiwa ndani ya kikosi cha Taifa Stars na kufanikiwa kumalizana na Tshabalala.

Kukamilika kwa usajili wa Tshabalala, sasa ataingia Yanga kuja kupambana na Mkongomani Chadrack Boka, huku ikiwa ni rasmi kutakamilisha mchakato wa Kibabahe kuwa nje ya hesabu za Yanga akitarajiwa kurejea Singida Black Stars.

Kibabage ana uhusiano ya karibu na bosi wa juu wa Singida, ambapo alikuwa tayari kumrudisha beki huyo akaungane na kocha wake wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi aliyeajiriwa hivi karibuni.