NAMUNGO imeendelea kusuka kikosi kwa kumalizana na aliyekuwa mshambuliaji wa TMA, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ kwa mkataba wa miaka miwili.
Mshambuliaji huyo amejiunga akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na TMA aliyoifungia mabao 18 msimu uliomalizika hivi karibuni na Mtibwa Sugar ikitwaa ubingwa wa Championship na kupanda daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, aliyekuwa kocha wa mshambuliaji huyo, Agustino Thomas alisema ni kweli amemalizana na Namungo akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba nao.
“Championship huwa tunasainisha wachezaji mkataba wa mwaka mmoja mmoja, hivyo Haaland ameondoka akiwa mchezaji huru na ametuma barua ya kuomba hati ya uamisho na kututhibitishia kuwa amepata timu nyingine ambayo ni Namungo,” alisema Thomas na kuongeza;
“Namungo wamefanya uamuzi sahihi kumsajili mshambuliaji huyo ni mchezaji mzuri na anajitambua nimemfundisha naelewa ukiangalia msimu huu akiwa na timu yetu amefungana na wachezaji wengine watatu kufunga mabao 18 hii ni wazi ni mpambanaji.”
Alisema anaamini mchezaji huyo atafanya makubwa katika kikosi hicho, juhudi na kujitambua ndiyo siri ya upambanaji wake na endapo atapata nafasi ndani ya timu hiyo utakuwa mwendelezo wa ubora wake.
Haaland kusaini mkataba wa miaka miwili katika timu hiyo anapishana na Meddie Kagere na Joshua Ibrahim ambao wamepewa mkono wa kwaheri baada ya kumaliza mikataba yao.