Dili la Mghana Tabora lakwama

DILI la beki wa kushoto wa Bibiani Gold Stars FC, Mghana William Ntori Dankyi kujiunga na Tabora United huenda likakwama rasmi, baada ya kudaiwa nyota huyo ameingiwa na tamaa ya kuhitaji kiasi kikubwa cha fedha tofauti na walivyokubaliana.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka uongozi wa timu hiyo, zimeliambia beki huyo aliyezaliwa Septemba 4, 1999, ni miongoni mwa pendekezo la benchi la ufundi, ingawa ugumu unatokana na kiasi kikubwa cha fedha anachokihitaji.

Hali hiyo imesababisha kutokuwa na maelewano mazuri ya mazungumzo na uongozi wa Tabora, ambao huenda ukaamua kaachana naye.

“Tulikubaliana Sh75 milioni za kumsajili na aliomba mkataba tumtumie ausome na tukamtumia pia, lakini ghafla tukashangaa anasema anataka zaidi ya kiasi hicho kitu ambacho siyo tuliyokubaliana mwanzoni,” kilisema chanzo hicho.

Kigogo huyo alisema kama beki huyo atashikilia msimamo wake, hawatokuwa tayari kuendelea na mazungumzo naye, badala yake wataangalia nyota mwingine mwenye uwezo mkubwa, kwa sababu machaguo yaliyopo bado ni mengi kikosini.

Bosi huyo alisema licha ya mkataba walioingia na moja ya kampuni kutoka Nigeria hivi karibuni wenye thamani ya zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa mwaka, ila watazitumia vizuri ili kutimiza chachu ya kutengeneza kikosi bora cha ushindani msimu ujao.

Hata hivyo, licha ya fedha hizo ila mabosi wa Tabora huenda wakaachana na mpango wa kumsajili Dankyi aliyezichezea timu za King Faisal FC, Hearts of Oak, Tema Youth SC, Liberty Professionals FC na Charity Stars FC zote za huko kwao Ghana.

Beki huyo msimu wa 2024-2025, aliisaidia Bibiani Gold Stars kuchukua ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya Ghana, ikishinda mechi 18, sare tisa na kupoteza saba kati ya 34 iliyocheza, ikiwa na pointi 63, huku ikifunga mabao 38 na kuruhusu 21.