Hassan Kibailo mbioni kutua Pamba Jiji

Pamba Jiji inafanya mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa beki wa kulia wa kikosi hicho, Hassan Kibailo, baada ya nyota huyo kudaiwa hayupo tayari kuendelea kuichezea Namungo na anaangalia sehemu ya kupata changamoto nyingine mpya.

Kibailo ni miongoni mwa nyota waliotokea mtaani na soka lake alilianzia huko katika timu ya Pasias Boys ‘Juma Kampong’ ya jijini Mwanza na baada ya hapo alienda katika akademia ya TSC na ndipo safari yake ya kisoka ikaanza kung’ara zaidi.

Mmoja wa kiongozi wa Pamba alilidokeza Mwanaspoti wanafanya mawasiliano na mchezaji huyo, ambaye ameonyesha utayari wa kukichezea kikosi hicho msimu ujao, hivyo mambo yaliyobakia ni madogo hususan suala la kukubaliana masilahi binafsi tu.

“Tunashukuru mchezaji mwenyewe ameonyesha utayari wa kuchezea Pamba, sisi pia kama viongozi tunapambana kuhakikisha kila kitu kinaenda vizuri ili kuepuka presha kubwa wakati dirisha la usajili litapokaribia kufungwa,” alisema kiongozi huyo.

Beki huyo aliyezaliwa Julai 23, 2000, akicheza timu mbalimbali za Coastal Union na Mtibwa Sugar, ni miongoni mwa nyota waliotokea katika timu za watoto wa mtaani na kwa sasa anaendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara hapa nchini.

Kama utakuwa umesahau, Kibailo ni miongoni mwa nyota wa Tanzania walioshiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa watoto wa mtaani na kutwaa ubingwa kwa kuichapa Burundi mabao 3-1 katika fainali iliyopigwa Rio de Janeiro Brazil, Aprili 7, 2014.