Shinyanga watumia saa 18 kusaka wawakilishi wa udiwani viti maalumu

Shinyanga. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekamilisha upigaji wa kura za maoni za uchaguzi wa ndani wa madiwani wa viti maalumu kwa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Kazi hiyo ilianza kufanywa jana Julai 20,2025 katika tarafa mbalimbali na kukamilika leo Jumatatu Julai 21, 2025 huku kundi kubwa la wanachama wakijitokeza kushiriki mchakato huo.

Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Mkoa wa Shinyanga, Salama Mhampi Saa tisa usiku wa kuamkia leo, amewatangaza waliopitishwa kwenye kura hizo za maoni huku akiwataka waendelee kuwa watulivu wakisubiri hatua inayofuata.

“Tarafa ya mjini jumla ya wagombea walikuwa 18 na waliopita ni watano ambao ni Moshi Kanji (536), Ester Makune (445), Veronica Masawe (431), Mwanakhamis Kazoba (355) na Eunice Manumbu (272, tarafa ya Old Shinyanga jumla ya wagombea walikuwa watatu aliyepitishwa ni Mwanaidi Sued kwa kura 539, tarafa ya Ibadakuli jumla ya wagombea walikuwa watatu mshindi ni Zuhura Mwambashi aliyepata kura 695,” amesema Mhampi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anord Makombe amewasisitiza viongozi hao pamoja na wajumbe, kuungana na kuachana na makundi ya mchakato wa kura za maoni ili kuimarisha mshikamano ndani ya chama,

“Ni muhimu kwa sasa kuacha tofauti, kujenga mshikamano na kuungana kama chama kimoja, hii ndiyo njia ya pekee ya kuhakikisha tunashinda kwa kishindo katika nafasi za udiwani na ubunge,” amesema Makombe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini, Rehema Nhamanila ametoa rai akisema, “naomba tusahau yaliyopita, tuvunje makundi na sasa tuungane kwa pamoja, ushindi wetu ni wa wote na tunahitaji kushikamana ili kuendelea kuimarisha UWT na CCM” amesema Nhamanila.