Musoma. Madiwani wa viti maalumu wanne kati ya watano waliokuwa wakitetea nafasi zao wamefanikiwa kushinda katika kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya CCM.
Madiwani hao wa Manispaa ya Musoma wamefanikiwa kurudi baada ya kuwa washindi wa pili hadi wa tano huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na sura mpya katika uchaguzi huo uliofanyika Musoma mjini jana Julai 20,2025.
Waliofanikiwa kurejea ni pamoja na Amina Masisa (465), Naima Minga (459), Herieth Kumira (440) na Asha Swaleh (421) huku mshindi wa kwanza katika kinyang’anyiro hicho Sister Yohana ambaye ni mgombea mpya akipata kura 510.
Akitangaza matokeo hayo saa nane usiku msimamizi wa uchaguzi huo, Baraka Mwachula aliwapongeza wajumbe kwa kukamlisha mchakato huo kwa amani na utulivu pamoja na uvumilivu wao.
“Niwapongeze kwa uvumilivu wenu tulianza mchakato saa nne asubuhi na hadi sasa saa 8.38 usiku bado mpo ukumbini, ni jambo jema kwamba tumemaliza salama sasa tusubiri taratibu nyingine ikiwa ni pamoja na vikao kwa ajili ya kukamilisha jambo hili kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema.