VIJANA NI CHACHU YA MAENDELEO ENDELEVU WAKIWEZESHWA NA KUWAJIBISHWA KIMAZINGIRA- KIKWETE

Maneno haya yamezungumzwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ndg. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akihutubia mkutano wa Vijana Wa Dunia katika Mji wa Suzhou, China.

Mkutano huo ambao ukutanisha vijana toka nchi mbalimbali duniani wakiwemo toka asasi za kiraia, mashirika ya kitaifa na kimataifa,na serikali mbalimbali ulibeba ujumbe unaosema Vijana ni Chachu ya Maendeleo Endelevu wapewe nafasi kuonyesha Uwepo wao, umekamilika kwa kutengeneza maazimio ambayo kila nchi iliyoshiriki mkutano itapaswa kuyaangalia ili kunyanyua ustawi wa vijana katika kushiriki ujenzi wa mataifa.

Mkutano huu ambao ulilenga pia kuangalia mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Malengo ya Millenia kwa upande wa vijana ulihudhuria na kuhutubia kwa njia ya mtandao moja kwa moja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ndg. Gilbert Houngbo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika Umoja wa Mataifa-UNFPA Nchini China Bi. Nadia Rasheed ambapo kwa pamoja walitoa msukumo kwa serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanatoa nafasi za kuwasikiliza na kuwahamasisha vijana kushiriki katika ujenzi wa sekta za maendeleo na kuwa wamoja katika kuyafikia malengo yao yakiwemo yale yanayowawezesha kuendelea.

Akihutubia Mkutano huo, Waziri Kikwete ameweka wazi hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa na serikali ya Awamu ya Sita ya Tanzania katika kuwawezesha vijana ikiwemo msisitizo mkubwa uliowekwa Kisera, kisheria na mipango mbalimbali ya kimaendeleo. Pia Waziri huyu wa Vijana alieleza na kuchambua vizuri hatua mbalimbali za mipango ya maendeleo na ushiriki wa vijana ikiwemo ile ya mgawanyo wa Asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri, Asilimia 30 za fedha za manunuzi ya umma,mikopo ya uwezeshaji wa Umma ikiwemo ya NEEC, BEST, na hatua ya kushusha riba kwa wakopaji katika mabenki ya biashara, uundaji wa Sera mpya ya Vijana nchini, Programu za maendeleo kama BBT-Madini, Kilimo, Mifugo ambazo zimeonyesha mafanikio makubwa kwa sasa.

Mkutano huo uliomalizika kwa mafanikio makubwa unakuwa ni mkutano wa 14 kukutanisha nchi wanachama na unafungua fursa kwa nchi wanachama , kukutana na kupeana uzoefu katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili vijana Duniani.