LICHA ya kuhusishwa kukaribia kujiunga na Yanga, aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah ameitosa ofa ya timu hiyo na kwa sasa inadaiwa amemalizana na matajiri wa Algeria, ES Setif FC na kusaini mkataba wa miaka miwili.
Nyota huyo aliyehusika na mabao 13, ya Ligi Kuu msimu wa 2024-2025 akiwa na Azam, baada ya kufunga mabao 11 na kuasisti mawili, ameamua kutafuta changamoto sehemu nyingine, huku Yanga iliyomhitaji pia ikikwaa kisiki kwa mabwenyenye hao.
Raia huyo wa Gambia alijiunga na Azam Julai 2, 2023, akitokea Raja Casablanca ya Morocco na kukitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili, akicheza jumla ya mechi 68 za mashindano yote, akihusika na mabao 31, baada ya kufunga 21 na kuasisti 10.
Nyota huyo aliyezaliwa Desemba 7, 1998, mbali na kuzichezea Raja Casablanca na Azam, ila timu nyingine ni Samger FC na Fortune FC za kwao Gwambia, Teungueth FC (Senegal) na Jeunesse Sportive Soualem inayoshiriki Ligi ya Morocco Botola Pro.
Sillah anakuwa ni mchezaji wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu huu kuhusishwa na Yanga na kutimkia Uarabuni, baada ya kiungo wa Singida Black Stars raia wa Ivory Coast, Josaphat Arthur Bada aliyehusishwa pia kudaiwa kutua JS Kabylie ya Algeria.
Awali Yanga ilidaiwa kukaribia kukamilisha usajili wa kiungo huyo ambaye ameitumikia Singida msimu mmoja tu na kuonyesha kiwango kizuri, tangu alipojiunga na miamba hiyo Agosti 1, 2024, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast.
Msimu uliomalizika wa 2024-2025, Bada alihusika na mabao 12, ya Ligi Kuu Bara akiwa na Singida na alifunga mabao manne na kuasisti manane, akiiwezesha kumaliza nafasi ya nne na pointi 57 na kufuzu Kombe la Shirikisho Barani Afrika.