Wananchi kuchangishana fedha kujenga shule

Simiyu. Wananchi wa Kijiji cha Nyashimba, Kata ya Ng’higwa, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, wameamua kuchukua hatua ya kujenga shule ya sekondari baada ya kilio cha muda mrefu kuhusu watoto wao kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wazazi na walezi waliokuwa wakilalamikia wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kulazimika kusafiri zaidi ya kilomita 20 kwenda shule za sekondari katika vijiji jirani, hali ambayo imekuwa ikisababisha baadhi yao kuchelewa masomo au hata kuacha shule.

Akizungumza katika mkutano wa kijiji uliofanyika Julai leo Jumatatu Julai 21, 2025, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyashimba, Balu Jiliya amesema wananchi wameamua kwa pamoja kuanzisha mchakato wa ujenzi wa shule hiyo.

Amesema lengo ni kuwaondolea adha watoto wao ya kutembea umbali mrefu kwenda Shule ya Sekondari Sukuma iliyoko Kijiji cha Mwadila.

“Tumeamua kwa moyo mmoja kujenga shule yetu ya sekondari. Tayari tumepata eneo la ujenzi na kila kaya inachangia Sh10,500. Hadi sasa tunayo matofali 6,000, pamoja na mchanga na kokoto,” amesema Jiliya.

Happines Sayayi, mkazi wa kijiji hicho amesema hatua hiyo imeleta faraja kubwa kwa wazazi waliokuwa wakihangaika kutafuta fedha za usafiri au kuwakodia nyumba za kuishi watoto wao maeneo jirani na shule ilipo.

“Wazazi tunapata shida kubwa ya kuwahudumia vijana wetu, wengine wanalazimika kuwapeleka watoto kwa ndugu ili waishi karibu na shule. Ila kwa makubaliano ya kuanza ujenzi huu, utatupunguzia gharama wazazi lakini hata watoto nao watapata mud wa kujisomea badala ya kuwaza kutembea kwenda shuleni,” amesema Sayayi.

Naye mkazi mwingine, Sayi Mipawa amesema wanatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao, hivyo hawawezi kusubiri hadi Serikali iwajengee shule.

“Tunajua elimu ni ufunguo wa maisha. Hatutaki kubaki nyuma kwa kutegemea kila kitu kutoka serikalini. Tumeamua kuanza wenyewe tukiwa na imani kuwa serikali itatuunga mkono baadaye,” amesema Mipawa.

 Ofisa Elimu wa Kata ya Ng’higwa, Jane Kidoto amesema kupatikana kwa shule hiyo kutakuwa mkombozi mkubwa, hasa kwa watoto wa kike ambao mara nyingi hukatisha masomo kutokana na vishawishi wanapokuwa safarini kuelekea shuleni.

“Hii ni hatua ya kishujaa. Shule hii itasaidia kupunguza mimba za utotoni, kuwapa wasichana nafasi sawa ya kupata elimu, na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla,” amesema Kidoto.

Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Yohana Simba amesema wananchi wanaendelea kuchanga fedha na kusomba mawe kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya awali, huku akitoa wito kwa wadau wa maendeleo, taasisi binafsi na serikali kuunga mkono jitihada hizo.

Mpango wa ujenzi wa shule ya sekondari Nyashimba unaonesha dhamira ya dhati ya jamii kuchangia katika kuboresha huduma za elimu, sambamba na juhudi za serikali za kusogeza elimu karibu na wananchi.