Ukisoma Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Tanzania imeupa mhimili wa mahakama, mamlaka ya utoaji haki na hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.
Sasa mhimili huu umetoa amri mbili na baadae Msajili akafafanua amri hizo kuwa ziliwalenga watu gani ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na kuibua sintofahamu kubwa kuhusu nani hasa wanaguswa na amri hizo.
Ni muhimu sana kama vile ilivyo mgonjwa na uji, kwa mhimili wa mahakama kujitokeza na kueleza umma, kuhusu nani yuko sawa kati ya Chadema, mawakili wa Chadema, mawakili wa waleta maombi na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu.
Pamoja na kile nitakachokieleza hapa na umbumbumbu wangu wa sheria, ninatamani Mahakama kama mhimili, ujitokeze na kusafisha hali ya hewa na kama kuna mahali imeteleza, basi itumie ‘suo motu’ kurekebisha dosari za kisheria.
Sio moto ni hatua inachukuliwa na mahakama yenyewe, bila ombi lolote la pande zinazohusika na amri au hukumu, kuchunguza kama kulikuwa na ukiukwaji wa sheria au makosa yanayostahili kusahihishwa kuepusha upotoshwaji wa haki.
Jambo hili lisipofanyika haraka, linaendelea kukanganya umma na linaweza kuharibu sifa nzuri na heshima ya mhimili wa Mahakama mbele ya umma.
Kilicholeta mkanganyiko ni tafsiri ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu juu ya amri ya mahakama kwenye maombi namba 8960/2025 yaliyofunguliwa na Said Issa Mohamed na wenzake dhidi ya Bodi ya wadhamini ya Chadema na Katibu mkuu.
Itakumbukwa kwamba Chadema kilifunguliwa kesi mahakama na makada wake wa upande wa Zanzibar, wakidai usawa kwenye mgawanyo wa mali za chama. Shauri hilo ni shauri namba 8323 na ilipangwa mbele ya Jaji Hamidu Mwanga.
Baada ya shauri la msingi kufunguliwa kuna maombi yalipelekwa mahakamani kupitia maombi namba 8960 ya 2025 ambapo waleta maombi katika shauri hilo walikuwa wakiomba zuio dhidi ya wajibu maombi kwenye kesi ya msingi.
Maombi hayo kama yanavyoonekana kwenye ukurasa wa pili wa maamuzi madogo ya Jaji Mwanga ya Juni 10, 2025 yanaomba nafuu tatu:-
Moja, wajibu maombi wazuiwe kwa muda kuandaa na au kushiriki kwenye shughuli zozote za kisiasa mpaka shauri husika litakapomalizika.
Mbili, wajibu maombi, wafanyakazi, mawakala, na yeyote anayefanya kazi kwa niaba ya wajibu maombi wazuiwe kwa muda kutumia mali za chama mpaka shauri husika litakapomalizika, tatu waliombwa walipwe gharama za maombi hayo.
Sasa maombi hayo yalisikilizwa na uamuzi ulitolewa na Jaji Mwanga na kwenye maamuzi yake, ukurasa wa 20, aliwapa waleta maombi ushindi kama walivyouomba isipokuwa kwa gharama za kesi aliachia kila upande ujigharamie.
Baada ya kutolewa kwa zuio hilo, mwezi mmoja uliopita, Makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche aliongea na vyombo vya Habari na kuwasihi wanachama wajitolee rasilimali zao ili kuendeleza shughuli za kisiasa za chama.
Kwamba kuachana na bodi ya wadhamini na Katibu mkuu ambao ndio waliozuiliwa basi wengine wote waendelee na harakati za chama.
Baada ya hotuba nilikuja kuona wanasheria wa waleta maombi kwenye shauri hilo wakieleza waandishi wa habari juu ya barua waliyomwandikia Naibu Msajili mahakama kuu Julai 2, 2025, ambayo imejibiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu masijala ndogo Dar es Salaam mnamo Julai 14, 2025.
Barua ya Naibu Msajili ambayo nimeiona na imesambaa mitandaoni, katika ukurasa wake wa 2 imetaja watu 10 ambao aya ya 4 ya barua yake inasema wanahusika na mazuio yote mawili yaliyotolewa na Jaji Mwanga.
Watu hao ni Bodi ya Wadhamini Chadema, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, makamu mwenyekiti Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, Katibu Mkuu Tanzania Bara au Naibu wake upande wa Zanzibar.
Wengine ni Viongozi wote na katika ngazi zote iwe ni viongozi walioteuliwa moja kwa moja katika nafasi zao za kiuongozi au wawe wana kaimu na mfanyakazi au wakala au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba ya Chadema.
Pia yeyote atakayefanya kazi kwa maelekezo au kuiwakilisha Chadema, atakayefanya kazi zozote za kisiasa kwa kutokea Taifa, mkoa, wilaya, Halmashauri, Tarafa na maeneo yote ya nchi kwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Taarifa hii ya Naibu Msajili imezua gumzo hasa baada ya mawakili wa Chadema kujitokeza na kuhoji juu ya uhalali wa Naibu Msajili kutoa tafsiri au ufafanuzi wa amri za mahakama ilihali amri hizo ziko wazi na kwa kingereza chepesi.
Chadema katika barua waliyomjibu Naibu Msajili wanadai Naibu Msajili hana mamlaka hayo na kwamba wanamtaka aombe radhi kwa alichokifanya. Tangu mvutano huu kuhusu tafsiri ujitokeze, Mhimili wa Mahakama uko kimya.
Katika tafakuri ya msuguano huo kuna mambo kama matatu nadhani ni muhimu yajadiliwe, moja ni je amri za mahakama zilihusu nini na nani alizuiwa na ipi?
Baada ya kusoma amri ile ya mahakama nimepata kuelewa mambo mawili, moja ni kwamba kuna shughuli za kisiasa na mbili kuna mali za chama.
Katika zuio la kwanza ni zuio dhidi ya kuandaa na kushiriki shughuli za kisiasa, zuio hili linahusu wajibu maombi ambao ni Bodi ya Wadhamini na Katibu mkuu.
Katika zuio la pili linahusu kutumia mali za chama, hili linahusu wajibu maombi na mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba yao. Kwenye hili la pili ni mwiko wao kusogelea na kuzitumia mali za chama.
Sasa amri ya shughuli za kisiasa ilihusu nani? Nianze kwenye hili na msemo wa kilatini wa kisheria unaosema “Expressio unius est exclusio alterius.”
Msemo huu wa kisheria una maana ya kwamba pale unapotaja jambo moja kama sehemu ya kitu unakuwa umetenga yale yote ambayo hukutaja.
Kwa kingereza wanasema the mentioning of one thing is exclusion of the other.
Sasa kwenye amri ya kwanza ya Jaji, inasema inawazuia Wajibu maombi kuandaa na kushiriki shughuli za kisiasa. Sasa amri ya kwanza haina maneno yanayowataja watu wengine kama ile amri ya pili inayotaja watu wengine.
Kwa uelewa wangu, Mahakama inaposema wajibu maombi inawaondoa watu wengine wote wasio wajibu maombi, na watu hao hawawezi kufungwa na amri hiyo. Huu ndio uelewa wangu mdogo nilionao katika masuala ya sheria.
Sasa swali la kujiuliza hapa, ambalo natamani mhimili wa mahakama ujitokeze na kutoa ufafanuzi ni kwamba je mahakama ingeweza kutoa amri dhidi ya wale ambao Naibu Msajili amewataja bila kuwasikiliza kama haki ya asili inavyotaka?
Nimefanya rejea ya maombi namba 64016 ya mwaka 2023, yanayomhusu Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG) na mwenzake dhidi ya Dhirajilal Walj Ladwa na wenzie wanne ambapo Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam katika ukurasa wake wa 22 inasema ifuatavyo na hapa naomba niinukuu kama ilivyo:-
“The principles of natural justice that we all cherish and subscribe to require, in one of its three pillars, that a person whose rights are affected by the decision to be taken by a judicial or quasi-judicial body must be afforded an opportunity to be heard.”
Kwa lugha nyepesi kabisa Mahakama ya Rufaa inasema mtu yeyote yule ambaye haki yake ya msingi inaathiriwa na uamuzi wowote ule wa mahakama au chombo cha maamuzi ni lazima apewe nafasi ya kusikilizwa.
Katika ukurasa wa 21 wa uamuzi wake katika rufaa hiyo, Mahakama ya Rufaa Tanzania inasema amri za mahakama sio barua ya kirafiki ambayo inaweza kupelekwa tu kwa mtu yeyote ambaye mleta maombi anamtaka.
Kwenye kesi hii Mahakama ya Rufani ilikuwa inaamua juu ya maombi yaliyoletwa mbele yake na AG yaliyokuwa yakipinga pamoja na mambo mengine maamuzi ya Mahakama Kuu kutoa amri dhidi ya mtu ambaye hakuwa sehemu ya kesi.
Hivyo kwa minajili hiyo bado najiuliza kama Mahakama Kuu inaweza kutoa zuio dhidi ya watu waliotajwa kwenye barua ya Naibu Msajili bila kuwasikiliza?
Kuna hoja ambayo nayo inajadiliwa sana mitandaoni na pia kwa baadhi ya wananchi, kama Naibu Msajili alikuwa na mamlaka ya kutafsiri amri ya mahakama au la, ambayo naamini mahakama ina wajibu wa kufafanua pia.
Majukumu na nguvu za Naibu Msajili zimetajwa kwenye sheria mbali mbali ukianzia kwenye Judicial Administration Act inayomtaja kama msaidizi wa Msajili na sheria ya mwenendo wa Madai (Civil Procedure Code sura ya 33 ya sheria za Tanzania) Amri ya 43(1) imeeleza yapi Naibu Msajili ana mamlaka nayo.
Hakuna hata moja linaloeleza kuwa ana nguvu ya kisheria ya kutafsiri Amri za mahakama, nami naamini hili ni jukumu la Jaji au majaji na ndio maana tangu mwanzo nimesema ni muhimu mhimili ukajitokeza kusafisha hali ya hewa.