Mtiania udiwani CCM aliyefia ajalini azikwa, Serikali yatoa salamu za pole

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita leo Jumatatu Julai 21, 2025 amewaongoza mamia ya waombolezaji kwenye maziko ya aliyekuwa Diwani wa Solwa aliyemaliza muda wake, Awadh Mbarak Aboud.

Aboud pia alitia nia kuomba ridhaa ya kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) unaoendelea nchini.

Akitoa salamu za pole kwa familia kwa niaba ya Serikali msibani leo Jumanne Julai 21, 2025, Mboni amesema kifo hicho kimewashtua, lakini hawana namna kwa kuwa kila mja wa Mungu, huondoka duniani kwa muda aupangao muumba.

Amesema kifo hicho ni pigo kwa familia, ndugu jamaa wa marehemu na wakazi wote wa Solwa, hivyo kila mmoja kwa imani yake amuombee pumziko la amani marehemu Awadh.

Awadh alifariki dunia jana Jumapili katika ajali iliyolihusisha basi la abiria la Kampuni ya Frester lililogonga bajaji na kuua watu wawili akiwamo diwani huyo. Ajali hiyo ilitokea eneo la Ibadakuli Barabara ya kuelekea Shinyanga mjini.

“Sote tunatambua hakuna mwenye kutambua muda wala saa, jambo hili limeshtua wengi kwa sababu hakuna mwenye kuondokewa na ndugu yake akapokea taarifa hiyo kwa urahisi, tuwatolee sadaka na kuwaombee dua njema kwa Mungu awapokee kwenye makao yake ya kheri,” amesema Mboni.

Akizungumza msibani hapo, Mbunge wa Solwa anayemaliza muda wake, Ahmed Salum amesema kifo cha Awadh kimeacha pengo kubwa kwa kuwa alikuwa mtu anayependa kuwatumikia wananchi na maendeleo kwa ujumla.

“Mdogo wangu Awadh ameacha pengo kubwa sana katika kata hii. Muda mwingi alikuwa akinisumbua kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya kata. Tunamuomba Mungu atuvushe salama katika nyakati hizi ngumu,” amesema Salum kwa masikitiko.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje amesema marehemu alikuwa kiongozi anayejituma kufuatilia miradi ya maendeleo ya kata pamoja na ushiriki wake katika vikao vya baraza la madiwani.

“Alikuwa mfuatiliaji mzuri sana wa miradi ya maendeleo ya kata. Pia alikuwa na mchango mkubwa katika kuchangia hoja zenye tija kwenye baraza la madiwani,” amesema Mboje.