SIMBA ambayo imeshaondokewa na wachezaji tisa wakiwamo wanne wa kimataifa na watano wazawa walioiotumikia msimu uliopita, inaendelea kujitafuta kwa kujipanga kimyakimya kwa kusainisha nyota kadhaa inayosubiri kuwatangaza hivi karibuni.
Simba iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipoteza kwa mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco, imeanza kusajili nyota wapya ili kujiandaa na msimu mpya baada ya kuachana na wachezaji tisa, wakiwamo wanane waliowapa ‘thank you’ na mmoja kumtoa kwa mkopo.
Wachezaji waliopewa thank hadi sasa ni Aishi Manula, Valentin Nouma, Kelvin Kijili, Hussein Kazi, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Fabrice Ngoma na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyetua Jangwani na kumrejesha kwa mkopo katika timu ya Mashujaa, kiungo Omary Omary.
Hata hivyo, wababe hao wa Msimbazi imedaiwa kupata ugumu kwa kubaniwa mastaa wawili na Azam FC, na fasta kuamua kumgeukia kiungo wa Yanga, Khalid Aucho.
Mabosi wa Simba walikuwa na hesabu za kumchukua Pascal Msindo ili awe mbadala wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amekitumikia kikosi hicho kwa muda mrefu wa miaka 11 baada ya mkataba wake kumalizika.
Hata hivyo, Simba ilifanya juhudi za kumbakiza beki huyo mkongwe lakini Yanga haikuiacha salama baada ya kuweka dau kubwa zaidi ya lile ambalo aliwekewa na wekundu, ikambeba.
Baada ya kushindwa kumshawishi kubaki huku jamaa akiaga rasmi, ndipo Simba ilipoamua kumgeukia Msindo ambaye ana mkataba wa miaka miwili na Azam, hivyo umamuzi huo uliwafanya wagonge hodi kwa mabosi wa Chamazi kutaka kumnunua.
Simba ilihitaji huduma ya mastaa wawili ambao wanacheza katika nafasi mbili ambazo ni beki wa kushoto (Msindo) na kiungo mkabaji Yahya Zayd, lakini ugumu ukaja kwenye dau walilowekewa mezani.
Kwa upande wa kiungo mkabaji, Simba ilikuwa na Fabrice Ngoma, Debora Mavambo na Augustine Okejepha ambao wameshapewa mkono wa kwa heri, huku Mzamiru Yassin mkataba wake ukiwa umekwisha, hivyo kama ataondoka atasalia Yusuph Kagoma pekee.
Mtoa taarifa kutoka ndani ya Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Tumeshindwa kuwa na nguvu ya ushawishi kumchukua Yahya Zayd na changamoto ni gharama ya kununua mkataba wake, lakini tunaangalia mpango mwingine.
“Kwa upande wa Msindo ambaye tulifikiria kama atakuwa mbadala wa Tshabalala, Azam wametuambia kama tunamtaka twende na Dola 300,000 (Sh781.7 milioni) na sio pungufu ya hapo, dau ambalo limekuwa kubwa.”
Kupitia Mwanaspoti, Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam, Zakaria Thabit, alisema klabu hiyo haina hesabu za kumuuza Msindo na wala hakuna timu ambayo imekwenda mezani kujadili dili hilo.
“Hakuna timu iliyokuja mezani kumtaka beki huyo kwani bado ana mkataba na bado hatuna mbadala wake licha ya kwamba tuna mastaa wengi ila huwezi kuuacha uzoefu wa Msindo,” alisema.
Baada ya kuona ugumu wa kumpata Zayd, Simba ikapata akili mpya na kugeukia upande wa pili kwa kiungo wa Yanga, Khalid Aucho ambaye amemaliza mkataba wake na mabosi wa Jangwani.
Mwanaspoti linafahamu kuwa, kiungo huyo na Yanga hawakufikia makubaliano kwa sababu mezani aliwekewa mkataba wa mwaka mmoja, huku yeye akitaka miwili.
Wakati akishindwana na Yanga, taarifa zinabainisha Aucho anahusishwa kutimkia nchini Israel kuungana na Kennedy Musonda waliokuwa wote Yanga ambapo nyota huyo hivi karibuni alitambulishwa kwenye kikosi cha Hapoel Ramat Gan.
“Aucho ana dili Israel kule alipoenda Musonda (Hapoel Ramat Gan), ila pia anahitajika na Simba, hivyo kuhusu kutua Simba bado anasita kufanya uamuzi wa kuendelea kucheza Tanzania,” alisema mtu wa karibu na Aucho.