WINGA wa kimataifa raia wa Gambia na Senegal, Lamine Diadhiou Jarjou ameandaliwa nyumba ya kishua pamoja na gari binafsi na Singida BS mara baada ya kufikia makubaliano ya kujiunga nayo kwa mkataba wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka katika klabu hiyo, mpango wa kumpatia Jarjou nyumba ya kishua na usafiri atakaokuwa anautumia kwa safari zake za ndani ulifikiwa mapema katika mazungumzo ya usajili, kama sehemu ya masharti ya kumvutia kujiunga na timu hiyo.
“Ni kweli kabisa, tayari ameandaliwa nyumba nzuri yenye kila kitu anachohitaji, pia tutampa gari ambalo litamsaidia katika shughuli zake binafsi akiwa Singida,” kilisema chanzo hicho.
“Huu ni mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha wachezaji wetu, wanakuwa katika mazingira bora.”
Jarjou mwenye umri wa miaka 23, amevunja mkataba wake na Grenoble Foot 38 ya Ligue 2 nchini Ufaransa ambao ulikuwa unatarajiwa kuisha Juni 2026, na uamuzi wake wa kuondoka unatajwa kuwa sehemu ya harakati za kutafuta nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Msimu uliopita, alicheza jumla ya mechi 22 katika mashindano yote, akifunga bao moja, kutoa pasi ya mwisho (asisti) moja, na kucheza kwa jumla ya dakika 845.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kocha mpya wa Singida BS, Miguel Gamondi, amevutiwa na uwezo wake baada ya kumuona kupitia ripoti za kiufundi na video za michezo aliyocheza akiwa Grenoble na klabu zake za zamani.
“Kocha Gamondi aliangalia kipande chake cha video, akasema huyu ni aina ya mchezaji anayehitaji mwepesi, anaweza kubeba mpira kwa kasi na kufungua nafasi kwa washambuliaji,” chanzo hicho kiliongeza.
“Baada ya hapo, menejimenti ilianza haraka kumfuatilia kwa ukaribu na mwishowe wakakamilisha kila kitu.”
Taarifa za ndani pia zinaeleza kuwa Singida BS ilianza mazungumzo na mchezaji huyo tangu Mei mwaka huu, lakini maamuzi ya mwisho yalifanyika Juni, muda mfupi baada ya mchezaji huyo kutangaza kuvunja mkataba wake kwa maelewano na Grenoble.
Jarjou, aliyewahi kung’ara katika klabu ya Casa Sports ya Senegal na timu ya taifa ya vijana ya Gambia na Al Hilal ya Sudan, anatarajiwa kuwa chachu mpya ya ushambuliaji wa Singida BS, ambayo imejipanga kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu msimu uliopita kwa alama 57.