BEKI wa pembeni wa Yanga, Kibwana Shomari amemtaja winga Maxi Nzengeli ni moja ya wachezaji wenye utimamu bora katika kikosi hicho na siyo rahisi kukabika.
Licha ya kwamba wanacheza timu moja, lakini ni miongoni mwa wakezaji ambao wakikutana mazoezini sio rahisi kumkaba na anamkubali kutokana na kupenda kazi anayoifanya.
“Unajua Yanga ni timu bora na ina wachezaji wengi wazuri, lakini Maxi ni mmoja wa wachezaji wagumu na wapo timamu, kumkapa unatakiwa kufanya kazi ya ziada kwani ana kasi na nguvu pia na huwa hakubali kushindwa kirahisi mazoezini kama uwanjani tunacheza mechi ya ushindani,” alisema na kuongeza;
“Namkubali na nimekuwa nikijifunza vitu kutoka kwake, licha ya kutokuwa na mambo mengi ni mchezaji bora na ni mtu wa kuzungumza na kila mmoja, kushauri na kutoa elimu juu ya nini tunatakiwa kufanya ili tufikie malengo.”
Akizungumzia nafasi yake Yanga baada ya kupoteza namba kikosi cha kwanza alisema hajawahi kukata tamaa na amekuwa akipambana bila kujua lini akipata nafasi na ndiyo maana akipata namba anaonyesha uwezo.
“Hakuna kazi isiyo na changamoto, kila kitu kinahitaji juhudi binafsi na kuamini kila kitu kinawezekana bila kujali shida iliyo mbele yako, ndicho ninachokifanya na ndiyo maana nikipata nafasi naonyesha,” alisema na kuongeza;
“Sijawahi kukubali kurudishwa nyuma na nimekuwa nikifanya vitu vya ziada ili kuwaonyesha watu mimi licha ya kukosa nafasi nilikuwa napambana na kuamini ipo siku nitaonyesha nikipata nafasi.”