‘Mzee wa kupeana’ afunguka dili la Rivers

ALIYEKUWA kipa wa  Fountain Gate FC, John Noble amerudi rasmi kwenye Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL) baada ya kujiunga na Rivers United kwa uhamisho huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake.

Noble, mwenye umri wa miaka 32, ni jina linalofahamika kwenye soka la Nigeria, hasa kwa mchango wake akiwa Enyimba FC mabingwa wa NPFL mara tisa na aliisaidia kutwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2023.

Ubora wake ulimfungulia milango ya kucheza nje ya nchi na mwaka huo huo alisajiliwa na Tabora United kabla ya kutua Singida Fountain Gate msimu wa 2024/25, ambao hata hivyo hakumaliza  kutokana na shutuma za kuhusishwa na upangaji wa matokeo.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kutua Rivers United, Noble alisema: “Nimerudi nyumbani kwa lengo moja kusaidia timu yangu mpya kufanya vizuri ndani na nje ya Nigeria. Najua presha iliyopo, najua matarajio ya mashabiki wa Port Harcourt, pia najua ninacholeta mezani uzoefu, uongozi, na roho ya ushindi.”

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Rivers United, klabu hiyo ilifanya maamuzi ya haraka kumchukua Noble mara tu baada ya kugundua ni mchezaji huru, wakiamini kuwa atakuwa nguzo muhimu kuelekea msimu unaokuja wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Noble tayari ameanza mazoezi na kikosi hicho, na ameonekana kuwa na hamasa kubwa ya kurejea katika viwango vyake vya juu, hasa baada ya kuwa na misimu miwili yenye changamoto nje ya Nigeria.

Rivers United, waliomaliza katika nafasi ya pili kwenye msimu uliopita wa NPFL, wanajiandaa kwa msimu mgumu wa mashindano ya CAF ambapo wanatarajia kupambana na vigogo wa soka la Afrika.