Nigeria. Katika tukio la kusikitisha mwanafunzi wa mwaka wa pili, Gloria Samuel (22) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kufuatia kuhusishwa na kifo cha mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Prince Abubakar Audu (PAAU), aliyekuwa naye hotelini.
Tukio hilo limetokea Anyigba, Kogi State nchini Nigeria ambapo asubuhi ya Julai 15, 2025, tovuti ya Daily Post Nigeria iliripoti kifo hicho cha mhadhiri huyo aliyefahamika kwa jina la Dk Olabode Ibikunle.
Kwa mujibu wa taarifa tukio hilo lilitokea katika moja ya hoteli mjini Anyigba ambapo kwa sasa Gloria amekamatwa na anashikiliwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai wa Jimbo (SCID).
Msemaji wa Polisi wa Kogi, William Ovye Aya, amethibitisha tukio hilo kwa Shirika la Habari la Nigeria (NAN) na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea.
Hata hivyo ripoti ya awali, inaeleza Dk Ibikunle alikunywa vinywaji vya kuongeza nguvu kabla ya tukio hilo. Imeelezwa alifariki dunia akiwa hospitalini alikowahishwa baada ya hali yake kubadilika.
Kulingana na meneja wa hoteli, Moses Friday, Gloria anayesoma chuo hicho cha PAAU alikimbia mapokezi kuwaambia wafanyakazi kuwa mhadhiri huyo alikuwa amezimia.
Mwanafunzi mmoja, ambaye alizungumza na NAN kwa sharti la kutotajwa jina kuhusu tukio hilo, alisema mhadhiri alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Gloria. Kwa mujibu wa tovuti ya Vanguard.
Imeelezwa Dk Ibikunle alikuwa kama mtu aliyejiandaa tendo hivyo kunywa chupa zaidi ya mbili za vinywaji vya kuongeza nguvu kabla ya kukutana kimwili.
Binti huyo anadaiwa kusema hakuwa na mawazo ya kumuua na kwamba hakumdhuru au kumpa sumu kwa njia yoyote. Hata hivyo, kutokana na mazingira ya kutatanisha yanayozunguka tukio hilo, polisi wanachunguza kesi hiyo kama mauaji ikisubiri matokeo ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (autopsy).
Vyanzo ndani ya polisi vinasema wachunguzi wanachunguza uwezekano wa mshtuko wa moyo uliosababishwa na matumizi mabaya ya vinywaji vya kuongeza nguvu. Kwa mujibu wa The Nigeria Education News.