Polisi yawasaka waliotelekeza boti yenye mirungi Tanga

Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawasaka watu wawili ambao bado majina yao hayajafahamika baada ya kutoroka na kutelekeza boti  ambayo ilibeba shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya, kuja Tanzania kupitia bahari ya Hindi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai 22,2025 mkoani humo na kueleza kuwa boti hiyo ilikamatwa na Kikosi cha Polisi Wanamaji katika eneo la Mawe Mawili Kijiji cha Kwale, mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga usiku wa kuamkia leo.

Amesema kuwa  watuhumiwa hao wametoroka baada ya kutelekeza boti yao aina ya fibre rangi nyeupe iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya, kupitia Bahari ya Hindi katika operesheni maalumu iliyofanywa na jeshi hilo katika kuthibiti dawa za kulevya.

Kamanda Mchunguzi, ameongeza kuwa watuhumiwa hao wawili waliokuwa kwenye boti walifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe, lakini boti pamoja na shehena ya mirungi vilikamatwa na vipo chini ya ulinzi wa polisi.

Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalumu hususan katika maeneo ya baharini ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahalifu kuvusha bidhaa haramu kutoka nchi jirani ikiwemo dawa za kulevya.

“Wale watuhumiwa walipoona boti ya polisi walianza kukimbia kufukuzana nayo, walipofika katika kisiwa cha Kwale waliruka na kukimbia, Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watuhumiwa hao na mmiliki wa boti,” amesema Kamanda Mchunguzi.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika jamii, hususan vinavyohusiana na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.

Aprili 5,2025 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya kaskazini, iliteketeza kiasi cha kilogramu 63.40 cha dawa za kulevya aina ya mirungi katika dampo lililopo eneo la Mahakama ya Wilaya ya Tanga.