Mabasi mapya 99 mwendokasi Mbagala kuwasili Agosti

Dar es Salaam. Ndoto ya wakazi wa Mbagala kutumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka inakaribia kutimia, baada ya mabasi 99 kuanza kusafirishwa kutoka China kuletwa nchini kutoa huduma hiyo.

Idadi hiyo ya mabasi yanayotarajiwa kuwasili Agosti 15, mwaka huu, ni sehemu ya yale 250 yatakayotoa huduma katika njia hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.

Hata hivyo, imepita takriban miaka miwili tangu Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ukamilishe utekelezaji wa miundombinu ya awamu hiyo inayohusisha eneo la Mbagala.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 20.3 kutoka Mbagala hadi Gerezani, ilijengwa na Kampuni ya Sinohydro kutoka China na ilikabidhiwa kwa DART tangu Agosti 2023.

Katika awamu hiyo, Kampuni ya kizalendo ya Mofat ndiyo imepewa mkataba wa miaka 12 kutoa huduma hiyo, na kwamba mabasi yake yatatumia nishati ya gesi asilia.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumanne, Julai 22, 2025, Mtendaji Mkuu wa DART, Dk Athuman Kihamia amesema baada ya kuwasili kwa mabasi hayo yatafuata mengine.

Mabasi hayo 99, amesema yameanza kusafirishwa kutoka China Julai 18 na yanatarajiwa kutumia siku 21 hadi kuwasili nchini Agosti 15, 2025.

“Julai 20, nilishuhudia mabasi 99 yakipakiwa pale China tayari kuanza safari kuja nchini. Tunatarajia yatafika hapa ndani ya siku 20 hadi 21,” amesema Dk Kihamia.

Ujio wa mabasi hayo utafuatiwa na mabasi mengine 101 yatakayoanza kusafirishwa Agosti kutoka China, kwa mujibu wa Dk Kihamia.

Mtendaji mkuu huyo amesema hayo yanafanyika kurahisisha huduma ya usafiri na kuwaondolea kero wananchi hasa wa Mbagala kuelekea Kariakoo, Posta na maeneo mengine.

“Kwa utafiti uliopo kutokana na wingi wa watu wa Mbagala kwenda mjini na Mbezi, kila siku mabasi makubwa 50 yenye urefu wa mita 18 yatakuwa yakianzia hapo safari zake ili kuwabeba abiria wote na kuondoa msongamano,” ameeleza.

Dk Kihamia amesema katika awamu hiyo ya pili, wamejipanga kuhakikisha changamoto zilizotokea katika awamu ya kwanza hazijirudii.

Hatua ya miundombinu ya awamu hiyo kukamilika mapema kabla ya kuwepo kwa mabasi, ilisababisha itumike vibaya na watumiaji wengine wa barabara, huku Dk Kihamia akitoa hakikisho kwa umma kuwa haitajirudia.

Baada ya mabasi hayo yote kutoka China, amesema vyombo vingine vya usafiri vitawasili nchini kutoa huduma katika barabara za Buza, Chamazi na njia za Kongowe na Vikindu.

Amesema hatua hiyo itawanufaisha watumiaji wa njia za Kimara na Gongolamboto.

“Tunaanza na magari 200, mambo ni mazuri, na tutatumia tiketi za kadi. Kwa Mbagala tumeagiza kadi milioni moja kwa ajili ya huduma hiyo,” amesema Dk Kihamia huku akigusia kwamba mabasi yatakuwa yanapita kila dakika mbili hadi tano.

Kwa sasa, DART inashirikiana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), ambalo ni mshauri katika utekelezaji wa mchakato wa awamu ya tatu na nne.

IFC inaendelea na hatua za mwisho za upembuzi yakinifu, maandalizi ya nyaraka za zabuni, kuratibu majadiliano na kuandaa mikataba.

Ili kuhakikisha uratibu unazingatiwa zaidi, DART ipo kwenye hatua ya kuajiri mshauri mwendeshaji wa mpito ili kuhakikisha mabasi yanakuwepo mara tu ujenzi utakapokamilika, huku uzinduzi ukitarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

“Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa zabuni. Baada ya kukamilika, mabasi yatawasili nchini yakiwa tayari kwa matumizi. Tutakuwa na nafasi ya kuyakagua kabla hayajafika, tofauti na awamu ya pili,” amesema Dk Kihamia

Katika kusisitiza hilo, Dk Kihamia amesema: “Suala la hali ya usafiri wa kugombania au kusubiria muda mrefu sasa litakuwa historia.”

Serikali imepata mkopo wa Sh570.6 bilioni kwa ajili ya kutekeleza awamu ya tatu na nne ya mradi huo. Kati ya fedha hizo, Dola milioni 148.1 za Marekani (zaidi ya Sh378 bilioni) zimepangwa kutekeleza awamu ya tatu, yenye barabara yenye urefu wa kilomita 23.6 kutoka Gongolamboto kupitia Barabara ya Nyerere hadi katikati ya Jiji, ikijumuisha sehemu ya Barabara ya Uhuru.

Mabasi hayo yanayokuja ni ya Kampuni ya Mofat iliyopewa zabuni ya kusimamia mradi huo. Julai 8, 2025, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Kampuni ya Mofat, Mabrouk Masasi akizungumza na Mwananchi alisema tathmini ya aina ya abiria imeshafanyika na wamehakikisha mabasi yanayotumika ni imara zaidi ili yasiharibike ndani ya muda mfupi.

Ndani ya basi hilo jipya, amesema vitatumika viyoyozi na hakutakuwa na utaratibu wa kufungua madirisha kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari.

Alisema wameweka zaidi ya Dola milioni 76 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh197 milioni, fedha zitakazotumika katika ufungaji wa mifumo yakiwemo mageti janja kwa ajili ya ukusanyaji wa nauli na shughuli nyingine za uendeshaji.

Naye, Mariam Juma, mkazi wa Kongowe, amesema huduma hiyo imekuja wakati muafaka, kwani eneo la Mbagala kwa sasa limekuwa kama kituo kikubwa cha watu kukutana wakitoka maeneo ya pembezoni, ikiwemo Chanika, Mbande, Chamazi, Kisemvule, Vikindu, na baadhi wakitokea mkoa wa Pwani, ikiwemo Mkuranga na Rufiji.

Kinachoendelea awamu ya tatu

Meneja wa Mradi wa BRT, Frank Mbilinyi, amesema awamu ya tatu imekamilika kwa takribani asilimia 90.

“Barabara kuu kutoka Gongolamboto hadi mjini zimeshakamilika kwa sehemu kubwa. Kilichobaki ni ujenzi wa njia za waenda kwa miguu na barabara za huduma ya dharura,” amesema.

Hatua hiyo ya kuja kwa mabasi hayo imepokelewa na wadau kwa matumaini huku wakitoa tahadhari kwa DART.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafirishaji (LATRA CCC), Daud Daudi, ametoa wito wa kuwepo kwa maandalizi thabiti ya uendeshaji na uhakika wa upatikanaji wa mabasi hayo.

“Watoa huduma lazima waweke kipaumbele katika matengenezo na upatikanaji wa mabasi. Moja ya changamoto kubwa katika awamu ya kwanza ilikuwa ni uhaba wa mabasi na mengine kuharibika mara kwa mara,” amesema.

Amesema matarajio yake ni DART kuhakikisha kunakuwa na mabasi ya kutosha kwa ajili ya njia ya Gongolamboto mara awamu ya tatu itakapozinduliwa.

Hofu kuhusu upatikanaji wa mabasi si jambo jipya. Awamu ya pili, iliyokamilika Desemba 2023, haikuanza kutoa huduma kutokana na kuchelewa kwa mabasi.

Hali hiyo ilisababisha mzigo kwa mabasi machache yaliyokuwapo kwa awamu ya kwanza.

Awamu ya kwanza ilizinduliwa ikilenga kuwa na mabasi 305, lakini idadi hiyo haijawahi kufikiwa. Mabasi mengi yaliyopo sasa ni mabovu. Kwa awamu ya pili, mabasi 755 yalipangwa kutumika, lakini yaliyonunuliwa ni 250.

Wakati DART ikisonga mbele na awamu ya tatu na nne, matarajio ni makubwa. Ikiwa sura hii mpya italeta mfumo wa usafiri wa haraka, kuaminika na kisasa, itategemea uwezo wa wakala huo kutimiza ahadi na kuzifanya kuwa matokeo halisi.