SUA yaanzisha programu sita za shahada za elimu ya amali

Morogoro. Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) kimeanzisha programu sita za shahada za kufundishia walimu masomo ya amali wa shule za sekondari nchini.

Lengo walimu hao watakapohitimu wawe na ujuzi na weledi wa kufundisha masomo hayo kwenye shule za sekondari.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Julai 22, 2025 na Makamu Mkuu Sua, Profesa Raphael Chibunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari cho hapo kuhusu kozi hizo.

Amesema mwaka 2024 Serikali ilifanya mabadiliko na kuanzisha elimu ya amali kwa shule ya sekondari, hata hivyo, changamoto iliyojitokeza ilikuwa ni uchache wa walimu wa kufundisha masomo hayo.

“Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilielekeza vyuo vikuu nchini kikiwemo SUA kuandaa mitaala ya kufundishia walimu wa masomo hayo ya amali na sisi tumeitikia na sasa tupo tayari kupokea na kufundisha walimu hao,” amesema Profesa Chibunda.

Amezitaja programu hizo ni shahada ya elimu ya uzalishaji wa mazao, shahada ya elimu ya ushonaji, shahada ya elimu ya bustani na mbogamboga, shahada ya elimu ya lishe na upishi, shahada ya elimu ya ufugaji viumbe wa majini na shahada ya elimu ya ufugaji.

Amesema SUA kina uwezo wa kufundisha walimu hao wa masomo ya amali na kimejiandaa kwa kuwa kina mashamba na vifaa vyote vya kujifunzia kwa nadharia na vitendo lengo ni kutoa walimu wenye weledi.

“Niwashauri vijana waliomaliza elimu ya kidato cha sita na wale wenye diploma waje kusoma, hizo programu zitawafanya waweze kupata ajira hasa katika kipindi hiki ambacho walimu wa masomo ya amali wanahitajika Kwa ajili ya kufundisha kwenye sekondari, lakini pia vijana wanaweza kujifunza ili waweze kujiajiri wenyewe,” amesema Profesa Chibunda.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Sua anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri wa kitaalamu, Profesa Maulid Mwatawala amesema programu hizo ni fursa ya ajira kwa vijana kwani wanaweza kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe.

“Elimu hii ya amali ina fursa ubwa kwani walimu watakaosoma elimu hiyo watakuwa na stadi kubwa ambayo wataweza kuajiriwa kufundisha kwenye shule za sekondari ama kujiajiri,” amesema Profesa Mwatawala.

Mkurugenzi wa kurugenzi ya shahada za awali kutoka Sua, Dk Hamisi Tindwa amesema vijana wanaotaka kusoma programu hizo wanaweza kufanya maombi kupitia tovuti ya chuo hicho na kwa wale ambao watashindwa kufanya maombi hayo kwa njia ya mtandao wanaweza kufika chuoni hapo Kwa ajili ya kupata usaidizi.