Mbeya. Licha ya Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kuwekeza ubora wa huduma ya viungo bandia na vifaatiba saidizi, bado kuna changamoto ya baadhi wagonjwa kushindwa kuzifikia kutokana na hali duni ya uchumi na ukosefu elimu hususani maeneo ya vijijijni.
Imeelezwa kuwa idara ya viungo bandia kwa mwaka ufikiwa na kutoa huduma kwa wastani wa zaidi ya wagonjwa zaidi ya 800 huku asilimia 40 mpaka 50 wakiwepo wanaume na watoto hunufaika .
Miongoni mwa mikakati ni kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii ya hospitali kufikisha taarifa za uwepo wa huduma za viungo bandia lengo ni kuona jamii yenye uhitaji inarejesha tabasamu.
Ofisa Mteknolojia Viungo Bandia na Mkuu ya Kitengo hicho, Beatrice Hankungwe amesema leo Jumanne Julai 2,2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital kuhusiana na hali ya utoaji huduma na mwamko wa wagonjwa kuzifikia hususani waliopata ajali za barabarani ili kurejesha tabasamu.
“Unajua huduma hizo zinalipiwa, lakini kuna wakati kuna wadau wanafika kusapoti nasi tunawatangazia wananchi mikoa ya Kanda yetu wanafika kuwekewa viungo bandia bure na kurejesha tabasamu wakiwepo watoto wadogo wanaobainika na changamoto za kuzaliwa,” amesema.
Ametaja miongoni na visababisha vya wagonjwa wanaofika kupatiwa huduma ya viungo bandia na vifaa tiba saidizi ni pamoja na wanaopatwa ajali saratani, kisukari, huku kundi kubwa ni wanaume.
Kwa upande watoto ametaja visababishi kuwa ni udhaifu wa mwili tangu wanapozaliwa hususani changamoto ya mtindio wa ubongo,mgongo wazi ,vichwa vikubwa na mengine yanayo husiana na hayo.
“Kimsingi kati ya asilimia 40 mpaka 50 ya wagonjwa tunao wahudumia wanaume ni wengi kuliko makundi mengine ,lakini tunatambua ni sehemu ya kundi ambalo ufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo uweza kusababisha ajali,” amesema.
Amesema wanaomba wadau kujitokeza kusaidia kulipia gharama kwa wenye mahitaji waweze kurejesha tabasamu kama jamii nyingine.
Katika hatua nyingine Beatrice, amesema elimu zaidi yahitajika kwa jamii kufuatia Serikali ya awamu ya sita kuwekeza katika kuboresha huduma za afya kwenye Hosptali ya Kanda ni wakati sasa kutumia fursa hiyo ili kurejesha tabasamu kwa ndugu na jamaa yenye mahitaji ya viungo bandia hususani miguu, mikono na matiti kwa wanawake.
Kwa upande wake, Ofisa mteknolojia viungo tiba na vifaa tiba saidizi Hosptali ya Kanda, Hemed Shalua amesema kutokana na elimu ndogo kwa jamii kuzifikia huduma wameweke mikakati mbalimbali ya kuwafikia hususani maeneo ya vijijini.
“Unajua furaha ya mwanadamu ni kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu ya utafutaji akiwa salama hivyo tunawasihi wenye changamoto kufika sambamba na kuomba Serikali kuongeza wataalamu kwenye idara hiyo kulingana na mahitaji,” amesema.
Sikitu Anthon Mkazi wa Iyunga jijini hapa,amesema ili wenye uhitaji kukimbilia huduma hizo ni vyema Serikali ingaanjia njia mbadala ya kusaidia kundi ambalo ukata umekuwa changamoto.
“Wapo watu mitaani anatambalia chini baada ya kupata ulemavu wa kudumu ambao hutokana na ajali, lakini kutokana na gharama za tiba analazika kuishi kwa matumizi kwa kukata tamaa ya maisha,” amesema.