Dar es Salaam. Familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya Kinondoni, Anna Hangaya, maarufu Mama Makete, imesema maradhi ya saratani ya mapafu ndiyo sababu ya kifo cha kada huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mama Makete ambaye ni mfanyabiashara amekuwa maarufu zaidi kutokana na kauli ya mahaba yake kwa CCM kwamba anaipenda kuliko wanavyowapenda watoto wake.
“Ukweli mimi nakipenda chama kuliko watoto wangu na watoto wangu wanajua hiki chama ni cha watu, sio chako kama huwezi kuishi na mwenyekiti wako vizuri ondoka, mliokalia nongwa mkubali yaishe chuki isiharibu jumuiya,” hii ni kauli ya kukumbukwa aliyowahi kunukuliwa Hangaya ambaye kwa sasa ni marehemu.
Hata hivyo, Mama Makete licha ya kusema anapenda sana chama alikuwa pia tajiri wa watoto, si kwa kuzaa tu, bali kwa kulea.
Msemaji wa familia Adam Mbyallu, ambaye ni mmoja wa vijana waliowahi kulelewa na Mama Makete, amesema marehemu enzi ya uhai wake aliwalea watoto zaidi ya 100 katika maisha yake, licha ya kuwa alizaa watoto wake watatu tu, wawili kati yao wakiwa wa kiume.
“Mama Makete alizaa watoto watatu, lakini alilea wengi mno. Mimi ni miongoni mwa watoto hao. Nimekulia katika nyumba hii pamoja na wenzangu zaidi ya 100. Kwa kweli alikuwa tajiri wa watoto kwa upendo wake wa kuwalea,” amesema Adam kwa hisia.
Akizungumzia sababu ya kifo cha Mama Makete, Mbyallu amesema maradhi ya saratani ya mapafu yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu ndio sababu ya kifo chake.
Amesema Mama Makete alifariki dunia jana mchana, wakati akiendelea kupatiwa matibabu kwenye Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI,) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu yanakoendelea maombolezo ya msiba huo, Mtaa wa Havanna Wazo Hill Kinondoni, Mbyallu amesema Mama Makete alikuwa akisumbuliwa na saratani ya mapafu yapata mwaka sasa na alikuwa anaendelea kutumia dozi ya dawa, ingawa dozi ya kwanza alikuwa amemaliza na kuanza ya pili.
“Baada ya kuanza dozi ya pili alikuwa anaendelea vyema na alikuwa ameanza kufanya shughuli zake kwa ufasaha, lakini yapata wiki tatu hivi zilizopita hali yake ya kiafya ilibadilika tulimrudisha hospitali kupata vipimo na ikabainika ile saratani bado inaendelea.
“Ndipo alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na kukatakiwa apelekwe Hospitali ya Ocean Road kwa matibabu, amepata matibabu kwa siku kadhaa yapata wiki kama mbili hivi hadi umauti ukamfika,” amesema.
Mbyallu amesema yeye, wazazi wake walitangulia mbele ya haki mapema, lakini Mama Makete aliwalea na alikuwa anawependa pamoja na kwamba alikuwa anakipenda chama chake.
Mbyallu amesema taratibu za kuupumzisha mwili huo zimeanza na zinaenda vizuri, maziko yanatarajiwa kufanyika Julai 24, 2025 kwenye boma lake lililopo Mtaa wa Havanna Wazo Hill.
“Mwili kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo, mwili utafikishwa hapa nyumbani Julai 23, 2025 jioni utalala na kufanyiwa ibada hapahapa kwenye boma lake,” amesema Mbyallu.
Pia, amesema wakati wa uhai wake, marehemu aliomba safari yake ya mwisho ikifika wala wasisumbuke azikwe kwenye hiyo nyumba yake katika sehemu ambayo tayari alishawaonesha na maandalizi yameshaanza kufanyika.
“Kaburi tumeshaanza kuchimba mapema kwa sababu eneo hili la Wazo kuna sehemu zina miamba mikubwa, tunahofia tukiacha siku moja ya maandalizi tunaweza kushindwa kukamilisha tunaamini hadi kesho tutakuwa tumekamilisha kuwahi hiyo Siku ya Alhamisi,” amesema Mbyallu.
Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Peter Bilebela amemzungumzia marehemu huyo, kama mtu aliyependa haki kutendeka wakati wa uhai wake.
“Naweza kumueleza katika maeneo mengi, lakini kubwa zaidi alikuwa mama anayependa haki zaidi, nakumbuka ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na hadi umauti unamfika alikuwa kiongozi na kulingana na nafasi yake alikuwa mjumbe wa Kamati za Halmashauri ya Kinondoni,” amesema.
Bilebela amesema alikuwa hapendi kuona mtu akionewa na alikuwa anapenda kuishi na watu vizuri hata kifo chake ni pigo kwa jamii nzima ya Nyakasangwe na wanakinondoni kwa jumla.
“Tumempoteza mtu katika kipindi ambacho tulikuwa tunahitaji msaada wake, alipenda watu na kuishi na watu vizuri kusikiliza watu lakini hatimaye Mungu amemchukua,” amesema Bilebela.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Ilala, Neema Kiusa amemuelezea marehemu wakati wa uhai wake alikuwa mama na zaidi ya kiongozi kulingana na umri wake na ukongwe wake ndani ya chama.
“Alikuwa na mapenzi ya dhati na chama na alipokuwa anaumwa tulikuwa tunapata fursa ya kuwasiliana naye, alikuwa anatueleza anaumwa lakini tuchape kazi ya kukijenga chama na kuunganisha wanawake ndani ya wilaya zetu kwa kutumia nafasi zetu,” amesema.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Ubungo, Sabina Mashauri amesema alikuwa mwenyekiti mwenzao lakini wanamkumbuka kwa mengi ikiwamo ujasiri na ukweli.
“Alikuwa mkweli, lakini sifa yake kubwa ni upendo na kwa Mkoa wa Dar es Salaam; yeye alikuwa mwenyekiti wetu kwa kutulea na alikuwa anasimamia anachokiamini na hakuwa muoaga, alitumia muda wake mwingi kuunganisha watu,” amesema.