CECAFA: Kujiondoa kwa Kenya kunahatarisha ari ya ushirikiano kikanda

Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesikitishwa na kitendo cha timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ kujitoa kwenye michuano ya CECAFA 4 Nation inayoendelea kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu mkoani Arusha.

Michuano hiyo imeanza leo Julai 22, 2025 kwa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuitandika Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes bao 1-0 lililofungwa na kiungo Idd Seleman dakika ya 17.

Jana Julai 21, 2025, Kenya ilitangaza kujiondoa kwenye mashindano hayo ambapo siku hiyo ilitakiwa kucheza shidi ya Taifa Stars.

Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Kenya (FKF), ilisema timu hiyo ilijiondoa kwenye mashindano hayo kufuatia mapendekezo na ushauri wa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Benni McCarthy baada ya kufanya tathmini ya kina juu ya mazingira yaliyokuwapo ambayo yalionekana hayafai kwa ushiriki wa timu na maandalizi ya jumla.

Kupitia taarifa iliyotolewa na CECAFA leo Julai 22, 2025, imeseama haikupendezwa na maamuzi yaliyofanywa na KFK licha ya kuwapa kila walichokitaka.

“Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) linasikitishwa sana na uamuzi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuiondoa Harambee Stars kwenye Mashindano ya Mataifa Nne ya CECAFA.

“Inasikitisha kwamba uamuzi huo ulikuja mnamo Julai 21 wakati masuala yote yanayofaa yaliyotolewa na FKF yalikuwa yameshughulikiwa mapema na CECAFA saa chache kabla ya kuanza.

“Katika mambo yaliyofanywa ni pamoja na kubadilisha hoteli ya timu ya Kenya kuwa mojawapo ya chaguo lao, kuhakikisha malazi kamili ya bodi na milo inayofaa kulingana na upendeleo wa lishe pia shirikisho lilihakikisha timu hiyo inawekewa huduma za internet kama lilivyoomba,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza.

“Hatua hizi zilichukuliwa kwa nia njema na kwa uharaka kuhakikisha wajumbe wa Kenya wana starehe na kuungwa mkono kikamilifu katika maandalizi yao.

“Tunaona ni muhimu kutambua kuwa timu nyingine shiriki za Uganda na Tanzania zilizofika Karatu kwa ratiba na zimekuwa zikitumia vifaa vilivyotolewa, licha ya kuonyesha kutofurahishwa na uandaaji wa mashindano hayo.

“Kwa hivyo CECAFA inaona kujiondoa kwa Kenya kuwa sio haki, haswa baada ya juhudi kubwa kufanywa ili kutimiza matakwa ya Shirikisho hilo.

“Hali ya ghafla ya kujiondoa inahatarisha ari ya ushirikiano wa kikanda na huathiri uadilifu wa mkutano wa maandalizi ulioundwa kwa kuzingatia maslahi ya pamoja ya timu zinazofungamana na CHAN.

“Mashindano hayo pia yalikubaliwa na Vyama Wanachama husika, na Mshirika wa Utangazaji wa CECAFA, Azam TV, kwa lengo la kutoa fursa ya mazoezi ya kui-giza mechi kwa timu.”

Mashindano hayo maalum ya CECAFA sasa yanahusisha timu tatu baada ya Kenya kujitoa, ambazo ni Taifa Stars (Tanzania), The Cranes (Uganda) na Simba wa Teranga (Senegal) ambapo Julai 24 Uganda itacheza dhidi ya Senegal na mchezo wa mwisho utawahusisha Taifa Stars dhidi ya Senegal Julai 27, 2025.