YANGA SC imeendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa 2025-2026 ambapo leo Juni 22, 2025 imemtambulisha winga, Offen Chikola.
Kwa mujibu wa Yanga, Chikola amejiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Tabora United.
Nyota huyo anakumbukwa na Wananchi kufuatia msimu uliopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara duru la kwanza kufunga mabao mawili wakati Tabora United ikishinda 3-1 dhidi ya Yanga.
Katika mchezo huo uliochezwa Novemba 7, 2024 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kilikuwa kipigo cha pili na cha mwisho kwa Yanga kwenye ligi msimu uliopita baada ya Novemba 2, 2024 kufungwa na Azam 1-0 uwanjani hapo.
Msimu uliopita, Chikola ndiye mchezaji aliyekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Tabora United baada ya kuhusika kwenye mabao tisa ndani ya Ligi Kuu Bara, akifunga saba na asisti mbili.
Winga huyo mzawa anakuwa mchezaji wa pili kutambulishwa rasmi ndani ya Yanga wakati huu wa usajili wa dirisha kubwa kuelekea msimu ujao 2025-2026 baada ya kiungo mkabaji Moussa Balla Conte raia wa Guinea aliyetokea CS Sfaxien ya Tunisia.