Hersi apita na mido wa Simba

ULISIKIA lile jina la kiungo Lassine Kouma kutoka Stade Malien? Yule aliyekuwa anawindwa na Simba? Basi Yanga imefanya kama ilivyofanya kwa mastaa wengine. Taarifa zinabainisha imeshapita naye jumlajumla.

Simba ilikuwa inampigia hesabu kiungo huyo, ikawa inapambana kuwania saini yake, ikipigania kununua mkataba wake wa mwaka mmoja.

Siyo Simba pekee, pia Al Hilal Omdurman ya Sudan, nayo ilikuwa imefikia pazuri ikibakiza hatua ya kukubaliana na mchezaji wakiwa wanabishana muda wa mkataba.

Wasudan hao walikuwa wanataka kumpa Kouma mkataba wa miaka mitatu na Dola 150,000 (Sh390.6 milioni) huku klabu yake nayo ikijiandaa kupokea Dola 120,000 (Sh312.5 milioni).

Klabu hizo mbili zote zikaachwa kwenye mataa, baada ya Kouma kumalizana na Yanga kimafia na mtu hatari alikuwa yuleyule, Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said.

Alichofanya Hersi, ni kutangulia kumalizana na mabosi wa Stade Malien, kisha alipopewa nafasi ya kumalizana na mchezaji, kila kitu kikamalizwa ndani ya saa 13 na dili hilo kufungwa.

Yanga jana, ilikuwa na kazi moja ya kutuma fedha kila upande kwenye dili hilo, ikijihakikishia usajili huo wa kiungo huyo mshambuliaji.

Kama humjui Kouma ni kiungo anayejua kuchezesha timu, pia ana ujuzi wa kufunga mabao kwa mashuti makali.

Kouma msimu uliopita ndiye alikuwa kiungo bora wa Ligi ya Mali, akihusika na mabao 16 akifunga saba na kutengeneza tisa.

Kukamilika kwa dili hilo, kunaifanya Yanga sasa kumchukua staa wa tatu ambaye alikuwa anapigiwa hesabu na Simba, kwenye dirisha hili la usajili akitanguliwa na Celestin Ecua na Moussa Balla Conte.

Mwanaspoti lilianza kuripoti Simba kuifukuzia saini ya Ecua kutoka Zoman FC ya Ivory Coast na  msimu uliomalizika alikuwa akiitumikia Asec Mimosas kwa mkopo huku akiibuka kuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast kabla ya Yanga kukamilisha dili lake lililothibishiwa na wakala wake.

Pia Mwanaspoti lilikujuza kuhusu Simba kumuhitaji Conte kutoka CS Sfaxien ambapo mchakato ulianza tangu Januari 2025 wakati timu hizo zilipokutana kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha wa Simba, Fadlu Davids akavutiwa naye, mwishowe ametambulishwa Yanga.

Ishu ya Kouma, pia Mwanaspoti limeripoti kwenye mazungumzo na Simba, japo hivi sasa taarifa mpya ni, amemalizana na Yanga. 

Wakati zoezi la usajili wa wachezaji wapya likiendelea ndani ya Yanga, pia klabu hiyo inafanya maboresho kwa kuwaongezea mikataba waliopo na klabu hiyo imetangaza kiungo Mudathir Yahya Abbas ataendelea kuwa kikosini hapo hadi mwaka 2027.

Hiyo ni baada ya kiungo huyo kuongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kusali katika kikosi hicho cha Yanga baada ya ule wa awali kumalizika mwisho wa msimu wa 2024-2025.

Mudathir alijiunga na Yanga Januari 2023 baada ya kukaa kwa takribani miezi sita bila ya timu tangu alipoachana na Azam FC mwishoni mwa msimu wa 2021-2022. Kumbuka nyota huyo aliitumikia Azam tangu 2012.

Akiwa Yanga, kwa misimu miwili na nusu iliyopita kabla ya kuongeza mkataba mpya, ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na mengine matatu ya Kombe la FA katika msimu wa 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025, sambamba na Ngao ya Jamii mara moja 2024.

Kuanzia msimu wa 2023-2024, Mudathir mwenye uwezo wa kucheza kiungo mshambuliaji na mkabaji, takwimu zinaonyesha amecheza jumla ya mechi 52 za Ligi Kuu Bara akifunga mabao 12 na asisti saba.