Tapa-HR watakiwa kuongeza weledi, kuondoa malalamiko kazini

Arusha. Wataalamu wa kada ya usimamizi wa rasilimali watu na utawala katika utumishi wa umma wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, kuepuka roho mbaya na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kupunguza malalamiko yanayotolewa dhidi yao kutoka kwa watumishi na wananchi wanaowahudumia.

Wito huo umetolewa leo, Jumatano Julai 23, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, alipokuwa akihutubia mkutano mkuu wa kwanza wa Jumuiya ya wataalamu wa kada hiyo (Tapa-HR) unaofanyika jijini Arusha.

Mhandisi Zena amesema baadhi ya watumishi wa kada hiyo wamekuwa wakilalamikiwa kwa tabia zisizozingatia maadili ya kazi na kusisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kujitathmini na kulinda taswira ya taaluma yao.

 “Tuendelee kusimamia kwa vitendo maadili ya utendaji kwa kujiepusha na rushwa na ukiukwaji wa maadili mahala pa kazi. Kwa kufanya hivyo, mtaondoa kero kwa wateja na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao,” amesema.

Ameongeza kuwa malalamiko haya hayawahusu wote, lakini wapo miongoni mwao wanaochafua taswira ya kada hiyo na kuifanya ionekane hasi katika jamii.

Aidha, amewataka wataalamu hao kuendelea kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali kazini ili kuongeza uadilifu, uwazi na uwajibikaji.

Kuhusu maendeleo ya taaluma hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi ameielekeza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana na wadau kuona namna ya kuanzisha Bodi ya Kitaaluma kwa wataalamu hao, pamoja na kuhuisha muundo wa maendeleo ya watumishi hao ili uendane na mahitaji ya sasa.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Xavier Daudi, amesema ipo haja ya wataalamu hao kubadilika kitabia na kiutendaji ili kuondoa mtazamo hasi dhidi yao.

 “Naamini baada ya mkutano huu tutakuwa tumebadilika. Natamani tutoke hapa tukiwa na jina jipya, tusitajwe tena kama watu wenye roho mbaya, bali kama wataalamu wanaochochea utekelezaji wa malengo ya taasisi zetu,” amesema Daudi.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Grace Meshy alisema mkutano huo wa kwanza umewakutanisha washiriki 999 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Amesema lengo la jukwaa hilo ni kubadilishana uzoefu, kukuza weledi na kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu katika sekta ya umma, huku akisisitiza kuwa wataalamu hao ni mhimili muhimu katika utekelezaji wa sera na ustawi wa taasisi za Serikali.

“Tutahakikisha tunaimarisha usimamizi wa rasilimali watu na kukuza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitia taasisi mbalimbali,” amesema.